Watu wanaoaminika kuwa majambazi waliokuwa na silaha za moto,
wamemuua mwenzao kwa kumpiga risasi usoni baada ya majambazi hao
kujichanganya wakati wakiwa katika harakati za kutoroka.
Habari zilizopatikana jana zilisema tukio hilo
lilitokea juzi saa 1:30 usiku eneo la Captown katika Manispaa ya Moshi
baada ya jaribio la majambazi hao kupora katika duka la simu kugonga
mwamba.
Habari hizo zilidokeza kuwa muda huo wakati
mmiliki wa duka hilo, Ramadhan Sauko akijiandaa kufunga duka lake,
waliingia watu wanne waliojifanya wateja na baadaye kumtolea bastola.
Hata hivyo, mfanyabiashara huyo alianza kupiga kelele za kuomba msaada
ambapo mmoja wa majirani aliamua kufyatua risasi hewani ambayo
iliwafanya majambazi watatu kukimbilia uchochoroni.
“Wakati wananchi wakijikusanya yule jambazi wanne
akakurupuka kutoka kule dukani akakimbilia kule uchochoroni kwa wenzake
na ndipo mlio wa risasi ulisikika uchochoroni,” alidai shuhuda mmoja.
Inadaiwa majambazi wale waliamini aliyekuwa
akiwafuata uchochoroni walikokuwa wamekimbilia kujificha alikuwa ni
mmoja wa wananchi waliojitokeza kutoa msaada na ndipo walipompiga
risasi. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
alipozungumza na wanahabari jana, alisema baada ya kusikika milio ya
risasi, alionekana mtu uchochoroni akiwa amejeruhiwa kwa risasi.
Kamanda Boaz alisema baada ya uchunguzi na
upekuzi, marehemu alitambuliwa kuwa ni Nicholaus Jacob Mushi (35), akiwa
na bastola aina ya Browning yenye namba 043916 ikiwa na risasi nane.
Bastola hiyo imetengenezwa nchini Czech na kusajiliwa nchini kwa namba TZ.TAR 73647.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, kumbukumbu za polisi
zinaonyesha marehemu alikuwa mhalifu mzoefu na alishawahi kuhukumiwa
kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kuvunja na kuiba.
Kamanda Boaz alisema Polisi linaendelea na
uchunguzi ikiwamo kuwatafuta watuhumiwa waliofanikiwa kutoroka kabla ya
mauaji ya mshirika wao huyo.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako