A

A

Katiba ya Tanganyika inawezekana kwa miezi mitatu

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akizungumza katika mkutano wake na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao 
********
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Katiba ya Tanganyika inaweza kuandikwa ndani ya miezi mitatu tu kwa kuwa maoni mengi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyozinduliwa Jumatatu, kwa kiwango kikubwa yametoka kwa wananchi wa upande huo wa Muungano.
Warioba alisema hayo jana wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kwenye Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
“Kutunga Katiba ya Tanganyika siyo kazi ngumu, ukisoma rasimu hii sura ya kwanza mpaka ya tano, sioni kama Katiba ya Tanganyika itakuwa tofauti na maoni yaliyomo katika sura hizo,” alisema na kuongeza:

“Misingi iliyopo katika utangulizi wa rasimu hii imetokana na maoni ya wananchi hao. Wakati wa kukusanya maoni, Zanzibar walijikita zaidi kwenye Muungano, maoni mengine kwa kiwango kikubwa yametoka kwa Watanzania Bara na katika kuandika Katiba ya Tanganyika sioni kama watabadilisha chochote kuhusu misingi hii ambayo ni; tunu za taifa, maadili, malengo na haki za binadamu.”
Alisema kuhusu kubadilishwa kwa mihimili ya Serikali na vyombo vingine vya kitaifa, kikubwa kinachoweza kuguswa ni muundo wa Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Baraza la Mawaziri.
“Kuhusu taratibu za kufanya kazi; iwe ni madaraka ya Rais, utaratibu wa kufanya kazi katika Bunge, Mahakama na Serikali sioni kama litakuja suala jipya kwa sababu mambo hayo yameshatolewa maoni. “Kilichobaki ni madaraka kwa umma tu, kwa maana ya Local Government (Serikali za Mitaa). Hata hili la madaraka kwa umma watakaolishughulikia watumie taarifa za wananchi waliotoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya. Wananchi walitoa maoni kuhusu jambo hili ambayo yapo wazi kabisa.”
Uchaguzi Mkuu 2015
Kuhusu uwezekano wa Katiba Mpya kutumika katika Uchaguzi Mkuu 2015, Jaji Warioba alisema Tume hiyo ilipewa muda mfupi wa kuandaa Rasimu ya Katiba kwa sababu ilielezwa kuwa uchaguzi wa mwaka 2015, utafanyika kwa kutumia Katiba Mpya.
“Katiba hii ilitakiwa iwe imekamilika Aprili mwaka huu, maana yake tungekuwa na mwaka mmoja na nusu wa kufanya mambo mengine ya kuwezesha itumike kwenye uchaguzi wa mwaka 2015,” alisema.
Alisema ndiyo maana katika rasimu hiyo, Tume imeweka masharti ya mpito ya miaka minne, kuanzia siku inapopatikana Katiba Mpya hadi Desemba 28, 2018.
Alisema rasimu hiyo imefafanua Baraza la Mawaziri na Bunge vitakuwaje… “Sasa hivi tuna Serikali na Bunge. Katiba Mpya itapatikana mwaka huu, lakini Bunge letu litaendelea kuwapo kwa msingi wa Katiba ya sasa mpaka ufike wakati wa uchaguzi, hiyo inafanyika kwa ajili ya kulinda uongozi wa Bunge na Serikali.”
Alisema ili kuwepo na Uchaguzi Mkuu kwa Katiba Mpya ni lazima itungwe Katiba ya Tanganyika, kwamba wamependekeza miaka minne ya mpito ili kutoa nafasi ya kubadilishwa kwa mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuundwa upya Tume ya Uchaguzi itakayoendesha uchaguzi kwa msingi wa Katiba Mpya
 
Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako