Rais wa mpito wa CAR ajiuzulu
Maelfu ya watu wamekimbia makwao kutokana na vurugu za kidini
Rais wa mpito wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati, Michel Djotodia, amejiuzulu
kufuatia shinikizo kali na kukosolewa kwa mwendo wake wa kujikokota
katika kusuluhisha mgogoro wa kidini unaotokota nchini humo.
Hatma ya Djotodia ilikuwa swala kuu katika ajenda ya mkutano wa viongozi wa kikanda kuhusu mzozo unaoendelea nchini humo.
Maelfu ya watu waliandamana leo katika barabara za mji mkuu Bangui kumtaka Rais Djotodia, ajiuzulu.
Rais Djotodia amekosolewa vikali kwa kukosa kumaliza mapigano ya kidini
kati ya wakristo na waliokuwa waasi waisilamu ambao walimsaidia kuingia
mamlakani kwa njia ya mapinduzi mwaka jana.
Baraza lote la mpito katika Jamuhuri ya Afrika ya kati limekwenda nchini
Chad ambako viongozi wa Afrika wanakutana kujadili mzozo unaoendelea
nchini humo.
Mkutano huo wa viongozi wa kikanda, uliahirishwa, mapema asubuhi Ijumaa.
Lakini wajumbe kwenye mkutano huo wanasema walitakiwa kuendelea na
mkutano usiku kucha ili kubuni mkakati kuhusu mustakabali wa Djotodia.
Viongozi wa kikanda wanasema wajumbe mia moja na thelathini na watano
waliitwa kwa mkutano huo kwa sababu ni raia wa nchi hiyo pekee wanaoweza
kuamua hatma ya taifa lao.
Ghasia baina ya wanamgambo wa kiisilamu na kikristo zimesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao.
Djotodia aliingia mamlakani baada ya mapinduzi ya kijeshi mwezi Machi
mwaka jana hali iliyotumbukiza taifa hilo katika viya vya wenyewe kwa
kwenyewe.