Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na Rais
Mstaafu Dkt. Amani Abeid Karume, wakionyesha kitabu cha Picha za
historia ya Zanzibar, baada ya kukizindua huko Makumbusho ya Mnazi
mmoja.
Mtunzi wa kitabu cha
Picha za historia ya Zanzibar Bw. Javed Jafferji, akitoa ufafanuzi wa
kitabu hicho kabla ya kuzinduliwa rasmi.
Baadhi ya mashuhuda katika uzinduzi wa kitabu cha Picha za historia ya Zanzibar,hafla iliyofanyika Makumbusho ya Mnazi mmoja.
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na mke wa
muasisi wa Mapinduzi Mama Fatma Karume wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Picha za historia ya Zanzibar kwa miaka 50 ya Mapinduzi.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, akizungumza katika
hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Picha za historia ya Zanzibar kwa miaka
50 ya Mapinduzi. (picha na Ali Hamad, OMKR).
Na Hassan Hamad OMKR
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesisitiza
haja ya kuendelezwa vipaji vya uandishi wa vitabu, ili kuwasaidia
wananchi kujua mambo mbali mbali yakiwemo ya kihistoria.
Mhe.
Maalim Seif ametoa wito huo katika viwanja vya makumbusho ya Mnazi
mmoja, wakati akizindua kitabu cha Picha za historia ya Miaka 50 ya
Mapinduzi ya Zanzibar, kilichoandikwa na mwandishi mzalendo Bw. Javed
Jafferji.
Amesema
iwapo vipaji vya aina hiyo vitaendelezwa, vitaweza kuibua vipaji
vyengine zaidi ambavyo vitapelekea kuitangaza Zanzibar na wazanzibari,
sambamba na kuendeleza kasi ya kukuza uchumi.
Amesema
kitabu hicho ni muhimu kwa Zanzibar, kwani kimeelezea nyanja mbali
mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii ambayo ndio sekta
kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar.
Akizungumzia
kuhusu miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Maalim Seif amewakumbusha
wazanzibari kuendeleza amani na umoja, ikiwa ni njia moja wapo ya
kumuenzi marehemu Mzee Karume na kuendeleza malengo ya Mapinduzi.
Amesema
Mzee Karume alikuwa mstari wa mbele katika kuhimiza umoja na maelewano
miongoni kwa wananchi, na kwamba ndio msingi wa maendeleo kwa nchi
yoyote duniani.
Amefahamisha
kuwa sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi zimekwenda sambamba na historia
ya Mapinduzi yenyewe ambayo yalifanyika siku ya Jumamosi kuamkia
Jumapili kama ilivyo kilele cha maadhimisho hayo mwaka huu.
Maalim
Seif ambaye ameshiriki katika kitabu hicho kwa kuandika Utangulizi
ambapo Rais Mstaafu Dkt. Amani Abeid Karume naye alishiriki kwa kuandika
dibaji ya kitabu, amesifu kazi kubwa iliyofanywa na mwandishi huyo ya
kukusanya picha muhimu za kihistoria ambazo baadhi yake ni adimu kwa
wazanzibari.
Kwa upande wake Rais mstaafu wa awamu ya sita Mhe. Dkt
Amani Abeid Karume amesema kitabu hicho kinaendeleza historia ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Amesema lengo la Mapinduzi ni maendeleo kwa wazanzibari wote,
na kwamba Wazanzibari wote ni wanamapinduzi na waumini wa Mapinduzi hayo kulingana na historia ya nchi ilivyo.
Mapema
mwandishi wa kitabu hicho Bw. Javed Jafferji amesema kitabu hicho
kilichomchukua muda wa mwaka mmoja hadi kukamilika kwake, kimekusanya
matukio ya kihistoria yakiwemo historia za watu mashuhuri.
Amesema alishajiika kuandika kitabu hicho baada ya kuona kinakidhi haja ya kihistoria kwa miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Naye
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk
amesema kitabu hicho kitakuwa chachu ya mafanikio katika nyanja mbali
mbali ikiwemo Utalii.
Amesema
mwandishi wa kitabu hicho amekuwa mshirika mkubwa wa Wizara ya Habari,
na kwamba wataendelea kushirikiana nae katika kazi zake ili aweze
kuchangia maendeleo ya Zanzibar kupitia taaluma hiyo ya uandihsi.
Uzinduzi
huo wa kitabu umekwenda sambamba na maonyesho ya picha za kitabu hicho
ambazo zitakuwepo katika makumbusho ya Mnazi Mmoja, na kuwataka wananchi
kutembelea makumbusho hayo kwa lengo la kujifunza. http://www.zanzinews.com