MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amesema anatarajia kuwasilisha maelezo
binafsi kuhusu, kauli ya Mwanasheria Mkuu aliyoitoa juzi bungeni dhidi
yake na kumuita muongo kuhusu suala la kuwa na orodha ya watu wanaodaiwa
kuficha fedha nje ya nchi.
Zitto,
aliyasema hayo bungeni juzi, ikiwa ni siku moja tu baada ya Mwanasheria
Mkuu (AG), Jaji Frederick Werema, kudai mbele ya Bunge kuwa Serikali
inashughulikia kisheria suala la Zitto kudanganya Bunge na Kamati kuhusu
majina ya watu walioficha mabilioni ya fedha Uswisi.
Akizungumzia
sakata hilo, Zitto alisema kwa sasa hataki kuzungumzia suala hilo, ila
ukweli wote ataubainisha kwenye maelezo yake binafsi ambayo
atayawasilisha wiki ijayo kwenye mkutano wa 14 wa Bunge unaoendelea.
“Nimeamua
hili suala nilizungumzie ndani ya Bunge, kwa hiyo tayari nimewasilisha
maelezo yangu kwenye Ofisi ya Bunge, na wameniambia kuwa nitapangiwa
kuwasilisha maelezo hayo wiki ijayo, kila kitu nitakibainisha siku hiyo,
sina zaidi,” alisisitiza Zitto.
Wakati
akitoa majumuisho ya mjadala wa taarifa zilizowasilishwa bungeni juzi,
ambazo ni taarifa ya Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Werema alisema
katika suala hilo, Zitto amezidi kuwa mzito.
AG huyo
ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kuchunguza madai ya
mabilioni hayo amesema ili kumalizia uchunguzi wa fedha hizo ameomba
Spika wa Bunge kuongezea kamati hiyo miezi sita.
Werema
alisema alishangaa kitendo cha Zitto kutaka suala hilo liangalie mfumo
na siyo majina ya watu walioficha mabilioni hayo. Alisema awali yeye
alishauri kuangalia mfumo wa uwekaji wa fedha hizo, lakini Zitto
alikataa na kusema anataka kutoa dukuduku kwa kutaja majina ya watu
walioficha fedha hizo.
Alisema
mwezi Februari Kamati ilikutana na Zitto na kuwaeleza kuwa ana taarifa
na nyaraka na kutoa masharti lakini aliondoka kwenda katika kambi ya
Jeshi ambako Kamati ilimfuata lakini bado aliwataka kukutana Dar es
Salaam.
Alisema Mei mwaka huu hadi aliposema hakuwa na jina wala akaunti ya mtu yeyote ambaye ana akaunti nje ya nchi kwa kiapo maalumu.
“Jambo
la kushangaza ni leo kudai Serikali haina dhamira na suala la walioficha
fedha Uswisi? Kwa kweli Zitto Kabwe ni mzigo na sasa tunaingia kufanya
kazi hiyo ya uchunguzi kama Serikali kwa kutafuta taarifa bila kumuonea
mtu,” alisema Werema.
--Habari Leo

No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako