A

A

Wafanyakazi wa JNIA wafikishwa mahakamani kwa shitaka la kuiba simu 120


Sophia Mwambe na Godfrid Kileche, TSJ, HabariLeo — WAFANYAKAZI wawili wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na mashitaka ya wizi.

Washitakiwa hao Daudi Mwenga (49) ambaye ni dereva wa Kampuni ya Swissport na Jackson Kituka (30), mkaguzi wa kampuni hiyo, walifikishwa mahakamani hapo jana wakikabiliwa na makosa ya wizi wa simu 120.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka, Cecilia Mkonongo mbele ya Hakimu Janet Kinyage kuwa washitakiwa
walitenda kosa hilo Novemba 11, mwaka huu katika ofisi za kampuni hiyo.

Mkonongo aliiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa waliiba simu 10 aina ya Nokia M-Horse zenye thamani ya Sh milioni 3.4, simu 30 aina ya Nokia 5200 zenye thamani ya Sh 338,100, simu 20 aina ya Nokia 2680 zenye thamani ya Sh 644,000 na aina nyingine za simu ambazo gharama yake ni Sh 740,600, zote zikiwa na thamani ya jumla ya Sh milioni 5.2 mali ya Hamis Chemchem.

Mwendesha Mashitaka Mkonongo alisema washitakiwa walitenda kosa hilo huku wakijua ni kosa kisheria. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 16, mwaka huu itakapotajwa tena.

Washitakiwa walirejeshwa mahabusu, kutokana kushindwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kutakiwa kuwa na wadhamini wawili, kila mmoja awe ni mwajiriwa na awe na fedha taslimu Sh milioni 2.9.

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako