Mkurugenzi wa Usimamizi wa Uchumi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi akitangaza bei mpya ya umeme jana katika
mkutano na waandishi wa Habari Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Umeme wa mamlaka hiyo, Anastas Mbawala. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA
Tarehe
11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liliwasilisha
maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA). TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia
67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1
Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015. Vilevile
TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme
kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko
ya thamani ya shilingi ya kitanzania. Aidha, TANESCO iliomba
kuidhinishwa viwango vya gharama za kuunganisha umeme vinavyozingatia
ruzuku inaliyotolewa na Serikali, na kuidhinishwa tozo mbalimbali kwa
huduma zitolewazo na TANESCO.
Kwa
mujibu wa TANESCO, kupitishwa kwa maombi haya kutaliwezesha Shirika (a)
kupata fedha za uendeshaji na uwekezaji wa miundombinu, (b) kulifanya
Shirika liweze kukopesheka na hivyo kuwezesha kupata mikopo yenye
masharti nafuu, (c) kuliwezesha Shirika kukabiliana na ongezeko la
mahitaji ya umeme kwenye Gridi ya Taifa, na (d) kuongeza uwezo wa
kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu iliyopo ili
kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa huduma za umeme wa uhakika
kwa wateja.
Itakumbukwa
kwamba bei za umeme zinazotumika hivi sasa ziliidhinishwa mwezi Januari
2012. Bei hizo zilipanda kwa asilimia 40.29 ikilinganishwa na maombi ya
TANESCO ambapo ilipendekeza bei zipande kwa wastani wa asilimia 155.
Sababu ilikuwa ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kulikosababishwa
na hali ya ukame katika maeneo yanayotiririsha maji katika mabwawa ya
kuzalishia umeme, toka mwaka 2011. Hali hiyo ilipelekea TANESCO
kulazimika kununua umeme kwa gharama kutoka kwa wazalishaji wa dharura
(Emergency Power Producers). Hali ya maji katika mabwawa ya kuzalishia
umeme bado sio nzuri na hivyo TANESCO itaendelea kununua umeme kutoka
kwa wazalishaji wa dharura (Emergency Power Producers).
USHIRIKISHWAJI WA WADAU
Kulingana na Kifungu Na. 19(2) (h) cha Sheria ya EWURA, Mamlaka ilifanya
Taftishi ili kupata maoni juu ya ombi la kurekebisha bei za umeme.
Ukusanyaji wa maoni ulihusisha pia mikutano minne (4) iliyofanyika
Iringa na Shinyanga tarehe 15 Novemba 2013, Bagamoyo tarehe 20 Novemba
na kuhitimishwa Dar es Salaam tarehe 22 Novemba 2013. Aidha, tarehe 6
Desemba 2013, EWURA iliitisha mkutano wa mwisho wa wadau wakiwemo
wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini(MEM), TANESCO, Shirika la
Umeme la Zanzibar (ZECO), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, Baraza
la Watumiaji na Baraza la Ushauri la Serikali, Umoja wa Wazalishaji wa
Saruji wa Afrika Mashariki, na kiwanda cha ALAF. Katika mkutano huo
EWURA iliwasilisha mwelekeo wa maamuzi kuhusu maombi ya TANESCO na namna
zilivyokokotolewa. Wadau walipewa fursa ya kutoa maoni yao kuhusu
mwelekeo wa bei na maoni yao yamezingatiwa katika kufikia maamuzi ya
mwisho.
UCHAMBUZI NA UAMUZI
Kwa kufuata sheria na kanuni zinazoelekeza kuhusu uchambuzi wa bei ya
umeme, EWURA ilifanya uchambuzi wa kifedha na kiufundi ili kubaini uwezo
wa TANESCO katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Uchambuzi
uliangalia utendaji wa Shirika la TANESCO katika miaka iliyopita na pia
iliangalia majukumu yanayoikabili TANESCO katika miaka mitatu ijayo.
EWURA imebaini kwamba hali ya kifedha ya Shirika la Umeme sio nzuri.
Shirika limeendelea kupata hasara, ambayo iliongezeka kutoka shilingi
bilioni 47.3 katika mwaka 2010 na kufikia shilingi bilioni 223.4
mwishoni mwa mwaka 2012. Pamoja na mapungufu ya kiufanisi, sababu kubwa
ya ongezeko la hasara ni kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa umeme
ambao TANESCO inanunua kutoka kwa wazalishaji binafsi. Hali hii
imelifanya shirika kushindwa kulipa madeni yake ya muda mfupi na ya muda
mrefu, ambayo yamelibikizwa na kufikia TZS 456.8 bilioni tarehe 22
Novemba 2013, hali ambayo inatishia uendelevu wa huduma ya umeme hapa
nchini.
Mamlaka imetumia Kanuni ya Ukokotoaji wa Bei kama ilivyopendekezwa na
AF-MERCADOS wakati wa kukokotoa mahitaji ya mapato ya TANESCO. Kanuni
hiyo inawezesha kukokotoa bei zinazolandana na gharama halisi kwenye
mfumo wa umeme na kuzigawa kwenye makundi ya watumiaji umeme, kadiri
kila kundi linavyosababisha gharama kwenye mfumo wa umeme kwa mujibu wa
mahitaji ya Sheria ya Umeme ya 2008 Kifungu cha 23(2)(f).
EWURA imejiridhisha kwamba, ufumbuzi wa matatizo ya kifedha ya TANESCO, unahitaji njia/mikakati miwili itekelezwe kwa pamoja:
kuongeza bei ya umeme ili kufikia bei inayokidhi gharama halisi (Cost Reflective Tariff); na
TANESCO kupata mkopo wa gharama nafuu ama ruzuku kutoka Serikalini ili kulipa limbikizo la madeni ya Shirika.
Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA, katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba
2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme
kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja, kama
ifuatavyo:
Kundi D1: Hili ni kundi la wateja wadogo wa majumbani, hasa
vijijini, ambao hutumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi. EWURA
imeongeza wigo wa mahitaji ya umeme na kufikia uniti 75 kwa mwezi, lengo
likiwa ni kuongeza idadi ya wateja wa TANESCO wanaoweza kulipa kidogo
kwa matumizi ya umeme kwa kiwango hicho, na pia kuwahamasisha kutumie
zaidi umeme. Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya
uniti 50 kwa mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja, kutoka
shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1: Hili ni kundi la watumiaji wakubwa wa umeme majumbani,
biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na kusaga nafaka, taa za
barabarani, mabango n.k. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 306 kwa uniti
moja, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 85 ya bei ya sasa. TANESCO
ilipendekeza ongezeko la shilingi 131.
Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji umeme wa kawaida ambao
hupimwa katika msongo wa volti 400, na ambao matumizi yao ya wastani kwa
mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 wateja wafanyabiashara kubwa, viwanda vya
kati. Bei ya nishati iliyoridhiwa ni shilingi 205 kwa uniti moja, sawa
na ongezeko la shilingi 73 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza
ongezeko la shilingi 145 ya bei ya sasa.
Kundi T3-MV: Hili ni kundi la wateja wakubwa kama viwanda vikubwa
waliounganishwa katika msongo wa kati (Medium Voltage). EWURA
imeidhinisha bei ya nishati kwa kiwango cha shilingi 166 kwa uniti moja,
sawa na ongezeko la shilingi 45 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza
ongezeko la shilingi 148 kwa uniti moja.
Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja wakubwa waliounganishwa
katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000 na zaidi) ikiwa ni
pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement. Bei iliyoidhinishwa ni
shilingi 159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 53 la bei ya
sasa. TANESCO waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa uniti moja.
Bei ya umeme itakuwa inarekebishwa kila baada ya miezi mitatu kulingana
na mabadiliko ya kiwango na bei za mafuta; mfumuko wa bei, mabadiliko ya
thamani ya fedha, na upatikanaji wa ruzuku toka Serikalini.
Vilevile, TANESCO inatakiwa kutekeleza miradi ya uwekezaji iliyoainishwa
kwa kutumia fedha zitakazokusanywa kutokana na bei zilizoidhinishwa.
EWURA inaweza kurekebisha bei ya umeme ya TANESCO kila mwisho wa mwaka
2014 na/au mwaka 2015 endapo TANESCO itashindwa kutekeleza miradi
iliyotajwa katika Jedwali husika. Marekebisho hayo yatatokana na
makadirio ya gharama za miradi ambayo haikutekelezwa.
Kutokana na matazamio ya kuwa na mabadiliko makubwa katika uzalishaji wa
umeme (generation mix) katika mwaka 2015 na kuendelea, kutokana na
matarajio ya kuongezeka kwa kwa upatikanaji wa gesi asilia, EWURA
itafanya utafiti kubaini gharama halisi (Cost of Service Study) ya
huduma ya umeme kwa wakati huo. Hivyo, bei zilizoidhinishwa zitatumika
mpaka mwaka 2016, kama utafiti unaotazamiwa kufanywa hautakamilika kabla
ya mwisho wa mwaka 2015.
EWURA ililinganisha bei za umeme kwa kila Uniti, katika nchi za Afrika
ya Mashariki, na kuona kuwa bado bei za umeme za Tanzania zipo chini
ukilinganisha na bei za katika nchi jirani kama inavyoonyeshwa hapa
chini, kwa makundi mbalimbali ya watumiaji umeme.
Pamoja na maamuzi hayo, Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA, pia iliagiza TANESCO kutekeleza yafuatayo:
kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo yenye gharama nafuu ("least cost
merit order") na kuwasilisha ripoti kwa Mamlaka katika kila mwezi
ikionyesha uzalishaji halisi na mpango wa uzalishaji kama
ilivyoidhinishwa na EWURA;
kuhakikisha kuwa zabuni za miradi ya uzalishaji umeme zinatolewa
kulingana na mahitaji kama ilivyoidhinishwa kwenye Mpango wa Umeme wa
Taifa (Power System Master Plan). Miradi yote mipya lazima ipatikane kwa
njia ya ushindani kwa kufuata Sheria ya Umeme, "Public Private
Partnership Act", Sheria ya Manunuzi ya Umma na Kanuni husika;
kuwasilisha ripoti kila baada ya miezi mitatu kuhusu viashiria vya
takwimu za ubora na uhakika wa umeme (supply and reliability) katika
misongo ya 11kV, 33 kV, 66 kV, 132 kV, na 220 kV kwa kila mkoa kwa ajili
ya uhakiki. Takwimu husika zinatakiwa kuonyesha jumla ya masaa mteja
aliyokosa umeme kwa kila njia ya umeme ("feeder"), kukosekana kwa umeme
kulikopangwa (planned outages), na ambao haukupangwa (unplanned
outages), idadi ya matukio ya kukosa umeme katika kila "feeder", idadi
ya wateja wanaohudumiwa na kila "feeder", idadi ya wateja walioathirika
na katizo la umeme katika kila "feeder" na kiasi cha umeme
kilichokosekana kutokana na katizo hilo (total unserved energy in kWh);
kuwasilisha kwa Mamlaka, katika kipindi cha miezi mitatu baada kuanza
kwa Agizo hilo la Mamlaka, mpango wa utekelezaji wa "Demand Side
Management Programme" ili uidhinishwe;
kupunguza kiwango cha upotevu wa umeme (technical and non-technical
losses) katika mtandao wa usambazaji kutoka asilimia 19 ya mwaka 2012
hadi asilimia 15.1 ifikapo mwisho wa mwaka 2015;
kubuni mikakati ya kupambana wizi wa umeme utokanao na uunganishaji
umeme usio halali, na kuondoa ucheleweshaji usio wa lazima katika
kutunganisha wateja wapya;
kuhamisha wateja walio katika kundi la D1 kwenda T1 endapo matumizi yao ya mwezi yatazidi uniti 75 kwa miezi mitatu mfululizo;
kuwasilisha kwa Mamlaka, kabla au tarehe 31 Machi, 2014, Mpango wa
kuwawekea wateja wake mita za LUKU na AMR ili kupunguza wateja
wanaotumia mita za zamani (conventional meters);
kuwasilisha kwa Mamlaka, kila baada ya miezi mitatu, taarifa/ripoti ya
ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wateja wake ili kuongeza mapato ya
Shirika;
kutoa elimu kwa wateja wake kuhusu haki na wajibu wa wateja kwa mujibu
wa Mkataba wa Huduma kwa Wateja na kushughulikia kero za wateja kama
inavyoelekezwa katika Mkataba husika na Kanuni za Umeme;
kuwasilisha kwa Mamlaka, maombi ya marekebisho ya bei yatokanayo na
mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na ubadilikaji wa thamani ya
fedha; Ukokotoaji wa marekebisho hayo utakuwa kama ulivyoainishwa
katika Kanuni za Kupanga Bei za Umeme za mwaka 2013 (Electricity (Tariff
Setting) Rules, 2013);
kuendelea kutoa taarifa kwa Mamlaka kuhusu hali ya kifedha na
kiundeshaji. Taarifa hizi zitatumiwa na Mamlaka katika kutathmini
utendaji wa TANESCO ikilinganishwa na mashirika mengine ya umeme katika
nchi jirani ili kuboresha utendaji wake. Tathmini hii pia itatumiwa na
Mamlaka katika kubaini uhalali wa maombi ya baadae ya kurekebisha bei;
kuwasilisha kwa Mamlaka, kabla au tarehe 31 Machi 2014, mpango wa utekelezaji wa kila sharti katika Agizo la EWURA.
Bei mpya za umeme zitaanza kutumika tarehe 1 Januari 2014. Ni matarajio
ya EWURA kwamba TANESCO watatumia fursa hii kutoa huduma bora zaidi za
umeme na kuhakikisha kuwa wanashughulikia malalamiko ya wateja kila
yanapojitokeza ili kurejesha imani kwa Shirika la Umeme la TANESCO.
AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako