Taarifa Rasmi Kutoka IKULU:Rais Jakaya Kikwete Awajulia Hali Waziri wa Fedha William Mgimwa na Ofisa Mwandamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jenerali Vicent Kariongo Mritaba Afrika ya Kusini
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtembelea Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa katika Hospitali
ya Kloof mjini Pretoria, Afrika Kusini, ambako Waziri huyo amelazwa
akitibiwa.
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi ya
siku tatu nchini Afrika Kusini alimtembelea Waziri Mgimwa jioni ya jana,
Jumanne, Desemba 10, 2013, baada ya kumaliza shughuli za jana za
Kumbukumbu ya Kifo cha aliyekuwa kiongozi mashuhuri wa Afrika Kusini,
Mzee Nelson Mandela.
Katika mazungumzo yaliyochukua kiasi cha robo saa, Waziri Mgimwa alimwambia Rais Kikwete: “Hali yangu inaendelea vizuri Mheshimiwa Rais na nakushukuru sana kwa kupata muda wa kuja kuniona. Inatia moyo na nguvu sana Mheshimiwa Rais.”
Naye
Rais Kikwete amemtakia heri Waziri Mgimwa ambaye amekuwa kwenye
hospitali hiyo kwa muda sasa na baadaye alipata nafasi ya kusalimia na
wana-familia wa Mheshimiwa Mgimwa ikiwa ni pamoja na mke wake na binti
yake mkubwa.
Wakati huo huo, Rais Kikwete juzi, Jumatano, Desemba
11, 2013, amemtembelea Ofisa Mwandamizi wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania, Jenerali Vicent Kariongo Mritaba ambaye amelazwa kwenye
Hospitali ya Mifupa ya Lynnmed Clinic iliyoko eneo la Lynnwood mjini
Pretoria.
Rais Kikwete amemtembelea Jenerali Mritaba akiwa njiani
kwenda Uwanja wa Ndege wa Kituo cha Jeshi la Anga la Waterkloof ili
aweze kupanda ndege kurejea nyumbani.
Kabla ya kuondoka nchini,
Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi 91 wa wakuu wa Serikali na
nchi waliotoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mzee Mandela na kutia saini
Kitabu cha Kumbukumbu cha Kifo cha kiongozi huyo ambaye hujulikana kwa
jina maarufu la Madiba.
Viongozi hao walikuwa wa kwanza kutoa
heshima zao za mwisho kwa mwili huo ambao utalazwa kwenye Ofisi ya Urais
wa Afrika Kusini zilizoko katika majengo ya Union Buildings, Pretoria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11 Desemba, 2013
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako