WATOTO WA MITAANI WANABAKWA SUMBAWANGA
Watoto kulawitiwa ili wapate hifadhi ya kulala
au kupewa chakula kizuri ni sehemu ya maisha ya baadhi ya watoto waishio
mitaani mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
Hii ni siri kubwa ambayo imejificha miongoni mwao,
ili uweze
kupata siri hii inakulazimu lazima ujenge uhusiano wa karibu na wa muda mrefu na watoto hao.
kupata siri hii inakulazimu lazima ujenge uhusiano wa karibu na wa muda mrefu na watoto hao.
Watuhumiwa wakubwa wa kuwaingilia kinyume na
maumbile watoto hao ni baadhi ya walinzi wanaolinda katika maduka ya
biashara na vijana waliowazidi umri; vitendo hivyo vinaonekana kushika
kasi.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwandishi wa
makala haya kwa miezi kadhaa, umebaini kuwa vitendo vichafu
vimesababisha baadhi yao kuathirika kisaikolojia hivyo kujikuta wakiona
jambo hilo ni la kawaida na hulifurahia.
Watoto hao hufanyiwa vitendo hivyo hasa kipindi
cha masika ambapo mvua huwa zinanyesha, maeneo ambayo hupendelea kulala
nyakati hizo kwenye majumba ambayo ujenzi wake haujamalizika (Mapagala)
huwa yanavuja maji ya mvua hivyo hulazimika kuyazikimbia kujisalimisha
popote.
Watoto wa mitaani
Baadhi ya watoto wa mitaani waliozungumza na
mwandishi walikiri kwamba ni kweli kuna tabia hiyo lakini ni kwa usiri
mkubwa kwani iwapo itabainika mtu anamlawiti mtoto mwenzao huwa
wanapambana naye.
“Unajua sisi tunawasaidia walinzi katika malindo
yao nyakati za usiku, tulishakubaliana kama kuna mwenzetu analawitiwa na
anakubali tutamtenga.
Wapo watoto wawili tayari tumewatenga katika kundi
letu kwa tabia ya kupenda kulawitiwa, sasa kama wapo wengine
tukiwafahamu nao tunawatenga hata wakipata matatizo hatuwezi kuwasaidia”
mtoto mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jose (siyo jina lake halisi).
Naye mtoto aitwaye Juma anasema kuwa
kinachowaponza watoto wengine ni tamaa na sio hifadhi ya kulala pekee
kwani wapo watoto ambao wamezitoroka familia zao kwa kisingizio cha
ugumu wa maisha na kukimbilia mitaani kufanya kazi ya kuombaomba ambapo
wamekuwa wakidanganyika kwa vyakula kama Chips na pombe katika baa za
usiku.
“Sisi wengine tupo huku mitaani kwa sababu
mbalimbali zikiwemo za kipato duni cha familia zetu, malezi mabaya kama
vile kulelewa na kina mama wa kambo ambao ni chanzo matatizo kwa sehemu
kubwa lakini sio sababu ya kukubali kulawitiwa.
Ila wapo wale wanaopenda pombe na chips ndio
wanajikuta wakishawishiwa na sio tu na walinzi lakini pia hata baadhi ya
watu ambao hutumia kisingizio cha ulevi wa pombe ili kufanya vitendo
hivyo,” anasema mtoto Maiko (siyo jina lake halisi).
Walinzi
Baadhi ya walinzi walihojiwa kwa nyakati tofauti
na mwandishi wa makala haya walikiri kwamba wapo wenzao wamekuwa na
tabia ya kuwaingilia kinyume cha maumbile watoto hao.
“Ni kweli wapo wenzetu wana tabia hii hasa mtaaa
wa Nyerere road (barabara ya kuelekea mkoani) na kuna tukio la mauaji
liliwahi kutokea ambapo kuna mtu alikuwa mlinzi anamlawiti mtoto usiku
wa manane akamshushia kipigo hadi kumsabishia kifo” anasema mlinzi mmoja
anayelinda mtaa wa Kiwelu ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Hata hivyo, mlinzi aliyejitambulisha kwa jina moja
la Peter alisema kwamba yeye binafsi hajawahi kusikia kama kuna baadhi
ya walinzi wanafanya vitendo hivyo na watoto ila anachofahamu ni walinzi
kuwahifadhi watoto hao kwa kuwapa eneo la kulala kwenye vibaraza vya
waduka wanayolinda hali ambayo huwasaidia pia kiulinzi.
Ongezeko la watoto hao na mikakati ya kuwadhibiti
Afisa maendeleo ya Jamii Manispaa ya Sumbawanga,
James Biseko anasema hivi sasa manispaa hiyo ina watoto wa mitaani 6872
ambapo kati ya hao 3268 ni wavulana na wasichana ni 3604 takwimu
zilizopatikana baada ya utafiti uliofanywa kati ya uongozi Manispaa hiyo
na Shirika la Pact - Tanzania.
Shirika hilo lilishirikiana na Manispaa hiyo
kutafuta takwimu hizo wakati wakianza kutekeleza mradi wa pamoja tuwalee
unaolenga kumtaka mwana jamii kutunza na kusaidia watoto hao.
Aidha, uchunguzi wa kina uliofanywa na mwandishi
mjini Sumbawanga, umebaini kuwa ongezeko la watoto wa mitaani ni kubwa
na linasababishwa na hali ya umasikini wa kipato unaozikabili familia
nyingi.
Hali hiyo inawalazimu wazazi kuzikimbia familia
zao hivyo watoto kulelewa na kina bibi wasio na uwezo kiuchumi na
kuwatumia watoto hao kama sehemu ya kujipatia kipato cha siku kwa
kupita mitaani kuomba fedha.
Anaeleza kuwa baada ya watoto hao kuzoea maisha ya
kuomba mitaani hulazimika kutorudi kwa walezi wao (bibi) zao, hivyo
hubaki mijini wakiendelea na maisha ya kuomba omba.
Anaeleza kwamba sababu nyingine ni migogoro ya
kifamilia na malezi ya wazazi wa kambo.Pia tamaa ya baadhi ya watoto
kupenda kukimbilia mjini wakifikiri maisha ni rahisi.
Kwa upande wake, Deo Mlwafi ambaye ni mratibu wa
mradi wa pamoja - unaotekelezwa na Pact - Tanzania kwa kushirikiana na
Shideph+ Mkoa wa Rukwa anasema kuwa wao jukumu ni kuijengea uwezo jamii
kupitia kamati za mitaa ili kamati hizo ziweze kuwasaidia watoto hao.
Kuhusu Maambukizi ya ukimwi.
Makamu mwenyekiti wa Shidepha+ taifa, Godfrey
Mwikala anaeleza kuwa watoto hao wapo katika hatari kubwa ya kupata
maambukizi ya Ukimwi kwa kuwa wamekuwa wakishiriki ngono isiyo salama.
“Si watoto wa kike wala wa kiume wote wapo kwenye
hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kuwa
wanashiriki ngono zembe, hawana elimu yoyote.
Nafikiri ipo haja ya kuwepo kwa mradi mwingine ya
kuwafikia moja kwa moja watoto hawa kuwahifadhi katika vituo maalumu,
kuelimisha kuhusu athari ngono zembe, kuwapima afya ili kuona namna ya
kuwasaidia maana mradi wa Pact - Tanzania unalenga kuwaisaidia lakini
kupitia ngazi ya jamii tu” anasema.
Mipango na Mikakati ya Serikali.
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto imekuwa na mipango na mikakati ya kuhakikisha kwamba
watoto wote wanastawi na kuwa na maisha bora kutokana na kupatikana kwa
haki zao za msingi ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushiriki
katika mambo yanayowahusu bila ubaguzi wa hali yoyote.
Hiyo ni sehemu ya mipango na mikakati ya Serikali
ambayo ipo kwenye maandishi, pasipo utekelezaji wa aina yoyote ile ndio
maana ongezeko la watoto wa mitaani ni kubwa, na hakuna wenye kuchukua
hatua si Serikali kuu, za mikoa wala wilaya huku taasisi zisizo za
kiserikali zilizoanzishwa kwa ajili ya kusaidia kupunguza tatizo hilo
zimekuwa zikiishia kujinufaisha zenyewe.
Baadhi ya wananchi wanashauri Serikali
kushirikiana na familia ili kuhakikisha wanakuwa na maisha bora, tofauti
na ilivyo sasa, kwani kuna idadi kubwa ya watoto wa mitaani.
Mkazi wa Sumbawanga, Julian Francis anasema wakati
umefika kwa Serikali kuwa na mkakati thabiti katika kutokomeza vitendo
hivyo vichafu; polisi wanatakiwa kufuatilia hilo.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako