A

A

KIM NI RAFIKI YETU, NA ABAKI KUWA RAFIKI YETU, LAKINI HAFAI KUENDELEA KUWA KOCHA WA TIMU YETU

Na Bin Zubery
NDOTO za Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kurudia kile ilichokifanya mwaka 1994 nchini Kenya katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge ziliyeyuka jana usiku baada ya kufungwa 1-0 na wenyeji, Harambee Stars Uwanja wa Nyayo, Nairobi, bao pekee la mshambuliaji wa Thika United, Clifton Miheso dakika ya nne kwa shuti la umbali wa mita 20, baada ya kupokea pasi fupi ya Alan Wanga na kumchungulia kipa Ivo Mapunda.

Stars sasa itawania nafasi ya tatu kwa mara ya pili mfululizo kwa kumenyana na Zambia ambayo nayo jana ilifungwa 2-1 na Sudan katika Nusu Fainali nyingine Uwanja wa County ya Mombasa, zamani Manispaa.
Hii ni mara ya pili mfululizo, kocha Mdenmark, Kim Poulsen anaiongoza Stars katika Challenge bila ya mafanikio, baada ya mwaka jana pia mjini Kampala, Uganda kufungwa katika Nusu Fainali na wenyeji, Uganda.
Matokeo haya yanakuja, wakati tayari Kim ameshindwa kuiwezesha timu ya Tanzania, Taifa Stars kufuzu kushiriki mashindano yoyote kati ya iliyowania tiketi zake tangu arithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen Mei mwaka jana.

REKODI YA KIM POULSEN STARS

Mei 26, 2012
Tanzania 0 – 0 Malawi (Kirafiki)
Juni 2, 2012
Ivory Coast 2 – 0 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 10, 2012
Tanzania 2 – 1 Gambia (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 17, 2012
Msumbiji 1 – 1 Tanzania (Tanzania ilitolewa kwa penalti kufuzu Mataifa ya Afrika)
Agosti 15, 2012
Botswana 3 – 3 Tanzania (Kirafiki)
Novemba 14, 2012
Tanzania 1-0 Kenya (Kirafiki)
Desemba 22, 2012
Tanzania 1-0 Zambia (Kirafiki)
Januari 11, 2013
Tanzania 1-2 Ethiopia (Kirafiki)
Februari 6, 2013
Tanzania 1-0 Cameroon (Kirafiki)
Machi 24, 2013
Tanzania 3-1 Morocco (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 2, 2013
Sudan 0 – 0 Tanzania (Mechi ya kirafiki Ethiopia)
Juni 8, 2013 
Morocco 2-1 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 6, 2013 
Tanzania 2-4 Ivory Coast (Kufuzu Kombe la Dunia)
Julai 13, 2013
Tanzania 0-1 Uganda (Kufuzu CHAN)
Julai 27, 2013
Uganda 3-1 Tanzania (Kufuzu CHAN)
Septemba 7, 2013
Gambia 2-0 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
...KOMBE LA CECAFA CHALLENGE Novemba 25, 2012 Tanzania 2–0  Sudan (Kundi B) Novemba 28, 2012 Tanzania 0–1 Burundi (Kundi B) Desemba 1, 2012 Tanzania 7-0 Somalia (Kundi B) Desemba 3, 2013 Tanzania 2-0 Rwanda (Robo Fainali) Desemba 6, 2012 Tanzania 0–3 Uganda (Nusu Fainali) Desemba 8, 2012 Tanzania 1-1 Zanzibar (Zanzibar ikashinda penalti 6-5)  Novemba 28, 2013 Tanzania 1-1  Zambia (Kundi B) Desemba 1, 2013 Tanzania 1-0 Somalia (Kundi B) Desemba 4, 2013 Tanzania 1-0   Burundi (Kundi B) Desemba 7, 2013 Tanzania 2-2 Uganda (Robo Fainali, Stars ikashinda kwa penalti 3-2) Desemba 10, 2013 Tanzania 0-1 Kenya (Nusu Fainali) 
Taifa Stars chini ya Kim, kwanza ilitolewa kwenye kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), ikatolewa pia kwenye kinyang’anyiro cha Kombe la Dunia na ikatolewa pia kwenye kinyang’anyiro cha tiketi ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).
Nakumbuka, wakati anapewa timu, Kim alisema lengo lake ni fainali zijazo za Mataifa ya Afrika- alikuwa sahihi kwa sababu wazi angehitaji muda kutengeneza timu na kuiandaa kwa ujumla.
Lakini kulingana na mwenendo wenyewe na hali halisi ya timu kwa ujumla, chini ya Kim huwezi kuona dalili za Tanzania kupata tiketi ya Fainali zijazo za AFCON. Neno rahisi ni kwamba mwenendo wa timu yetu mbele ya Kim si mzuri, kiasi kwamba hata yeye mwenyewe anaonekana kabisa kuanza kukata tamaa.
Mbaya zaidi, hata wadhamini wa timu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) nao wanaonekana kuanza kukatishwa tamaa na timu hiyo chini ya Kim- si hadi Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe aseme, lakini dalili zinaonekana.
Mwaka jana katika Challenge ya Uganda, TBL walituma mwakilishi wake kuwa bega kwa bega na timu kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwenye mechi zote, lakini safari hii hawakuwa tayari kuchoma moto fedha zao kwa ajili ya timu ya Kim.
Nimesema mbaya zaidi wadhamini wanaonekana kuanza kukatishwa tamaa na timu yetu ya taifa pia chini ya kocha Kim, kwa sababu udhamini ndiyo uti mgongo wa timu, bila ya hivyo hali itakuwa mbaya zaidi na timu hiyo itakuwa mzigo kwa kila mtu.
Achana na madudu haya ya CECAFA Challenge, hadi sasa kocha Kim ameiongoza timu yetu ya taifa, Taifa Stars katika mechi 16 na kuambulia ushindi katika mechi tano, kufungwa saba na sare nne. 
Inauma zaidi tulifungwa na Uganda nyumbani na ugenini kuwania tiketi ya CHAN na kila siku Kim amekuwa akilia na wachezaji na amekuwa akibadilisha vikosi mara kwa mara. Ameachana na makipa aliokuwa nao tangu aanze kazi, Juma Kaseja na Mwadini Ally na kuwachukua Ivo Mapunda na Deo Munishi ‘Dida’ na amekuwa akibadilisha wachezaji atakavyo. Hakuna anayemuingilia, kwa sababu watu wanataka matokeo tu.
Sasa jitihada zake zote, matokeo yake ndiyo haya ambayo tunayaona sasa na huwezi kusema kingine, hata kama Kim ni kocha bora kiasi gani, mchapa kazi wa aje, kwa kuwa matokeo ya timu yetu si mazuri, basi hatufai. Binafsi, nampenda Kim, napenda sera zake napenda namna anavyofanya kazi. Jamaa ni hodari sana. Lakini sioni matunda ya kazi yake!    
Rejea CECAFA Challenge ya mwaka huu, Kim atatoa kisingizio gani? Aliita timu mbili zikawekwa kambini zote, timu ya chipukizi, Future Taifa Stars na ya wakubwa, Taifa Stars ambazo baadaye zilimenyana ili ateue wachezaji wa kuja nao Challenge. Kutokana na mechi ambayo Future waliwafunga kaka zao 1-0, Kim akateua kikosi cha Challenge.
Bahati iliyoje kwake, TP Mazembe nayo ikawaruhusu Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kuja kuichezea timu ya Kim- kwa hivyo alipata kila alichokihitaji na matokeo yake tukafungwa 1-0 katika mchezo ambao tungeweza kushinda kama si upangaji wake wa timu usioeleweka. Kuna wachezaji anawang’ang’ania kikosini huwezi kuona kwa sababu gani, wakati anawaacha wachezaji bora.
Tazama mabadiliko aliyoyafanya jana, alimtoa Amri Kiemba akamuingiza Farid Mussa, ambaye alishindwa kabisa kucheza, kila pasi akipelekewa ilikuwa mpira unatoka nje. Lakini ukirejea nyuma, kuna wachezaji ambao tayari Kim alikwishaanza kuwajengea kujiamini katika mashindano haya tangu hatua ya makundi, akina Haroun Chanongo na Ramadhani Singano ‘Messi’ na ambao pia wanamzidi uzoefu Farid.
Kufungwa si kitu, suala ni namna ambavyo mnafungwa- Chanongo alimfungia bao Kim katika mechi na Somalia na bado ameonekana kucheza vizuri akiwa pamoja na Messi, jana baada ya kuona aliowategemea wameshindwa, kwa nini asiwaingize hao vijana?  
Ile ilikuwa mechi kubwa, Kim alimuonea Farid na mbaya zaidi kwa sababu mechi ilikuwa imekwishachafuka- afadhali angemuingiza katika mchezo ambao Stars ilikuwa inaongoza. Sasa, matokeo yake badala ya kumjenga mchezaji huyu chipukizi mwenye kipaji, Kim anajikuta anachangia kumbomoa. Wachezaji wadogo huwa wanainuliwa taratibu na si kama anavyotaka kufanya Kim.
Lakini pamoja na yote, bado huwezi hata kufurahishwa na mfumo wa uchezaji wa Stars, ndiyo kuna wakati zinapigwa hata pasi thelathini, lakini zisizo na malengo wala mipango zaidi unaweza kuona mabao yanatokana na juhudi binafasi za wachezaji. Kwa kweli bila kuoneana haya, Kim ni rafiki yetu, na abaki kuwa rafiki yetu, lakini hafai kuendelea kuwa kocha wa timu yetu. Jumatano njema. 

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako