HALMASHAURI ya Manispaa Tabora inatarajia kutenga jumla ya hekta 14 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa hiyo, Alfred
Luanda kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya hiyo (DCC)
kilichoketi kwenye ukumbi wa manispaa hiyo.
Luanda alisema awali manispaa ilitenga eneo la ujenzi wa hospitali
hiyo karibu na kambi ya Wachina, lakini kiwanja hicho kilikuwa hekta
6.2 huku ramani iliyotoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) inahitaji kuwa na hekta 12.
Alisema waliamua kukaa kama menejimenti ili kuomba eneo la Shule ya
Sekondari Wasichana Tabora kwa kuwa kuna eneo lenye ukubwa wa hekta 97.
Luanda alisema baada ya kutembelea na kuliona eneo hilo, waliomba
hekta 14 hasa kwa kuzingatia baadhi ya wavamizi wameanza kuingia katika
eneo hilo.
“Kutokana na mchakato huo, hakuna ofisi yoyote waliyokwenda kupata
ushauri wa maamuzi hayo na ndipo kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na
usalama wilaya waliafikiana suala hilo,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kikao cha Baraza la Madiwani pamoja na
cha Bodi ya Shule ya Sekondari wasichana Tabora waliunga mkono hatua ya
kumega eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Chanzo;Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako