A

A

Fahamu Kuhusu Kuachiwa huru kwa Watuhumiwa wakumwagia Sumu na kuharibu Ekari 557 za Wananchi,Mbeya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mbeya, imewaachia huru watuhumiwa watatu ambao ni Mwekezaji wa Shamba la Kapunga(Kapunga Rice Project) lililopo Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya ambao walikuwa wakituhumiwa kwa mashtaka matatu ambayo ni kula njama, kumwaga sumu na kuharibu mashamba ekari 557 ya Wananchi.

rubani wa ndege Andreas Daffee. akipongezana na wakili wake Lweikaza
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mbeya, imewaachia huru watuhumiwa watatu ambao ni Mwekezaji wa Shamba la Kapunga(Kapunga Rice Project) lililopo Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya ambao walikuwa wakituhumiwa  kwa mashtaka matatu ambayo ni kula njama,  kumwaga sumu na kuharibu mashamba ekari 557 ya Wananchi.
Akisoma hukumu Mhakamani hapo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili watuhumiwa ambao ni Waldeman Veemark ambaye ni meneja wa shamba, Sergei Beacker ambaye ni Afisa Ugani wa kampuni pamoja na rubani wa ndege Andreas Daffee.
Mteite alidai kuwa mbali na upande wa mashtaa kuwa na mashahidi 155,ambapo kati yao mashahidi zaidi ya 20 hawakuweza kufika mahakamani huku wengine 9 wakitoa ushahidi wa uongo tofauti na mashtaka yaliyopelekwa.
Aliongeza kuwa katika mashahidi hao, Shahidi wa 102 ambaye ni Mtaalam wa  Kilimo wa kijiji cha Kapunga aliyefahamika kwa jina moja la Geophrey alishindwa kuithibitishia Mahakama utaalamu wa kimaabara kwamba kilichomwagwa na watuhumiwa hao ni sumu.
Hakimu huyo alisema pia mashahidi hao zaidi ya 100 hakuna aliyekiri kuwaona washtakiwa wakitenda kosa hilo licha ya kudai waliiona ndege ikiwa angani  ikinyunyiza vitu vinavyodhaniwa kuwa ni sumu.
 
Kutokana na ushahidi huo Hakimu Mteite alisema Mahakama inawaachia huru washtakiwa wote watatu kwa mujibu wa kifungu cha 312 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. 
Awali mwendesha mashtaka wa Serikali, Archiles Mulisa alidai mahakamani hapo kuwa Watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Januari 12, 2012 kinyume cha sheria namba 336 na kifungu cha 122(i), sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Ambapo walidaiwa kuharibu ekari 557.5 za mashamba ya mpunga ya wananchi yenye thamani ya shilingi zaidi ya Milion 800 kwa kumwaga dawa inayodaiwa kuwa ni sumu kwenye maji na mazao hali iliyowaathiri kiafya baadhi ya wananchi.
 
Kwa upande wa washtakiwa ambao walikuwa wakitetewa na Wakili Ladislaus Lwekaza, ambapo wakiwawanajitetea walisema kwamba hawakuhusika na tukio hilo na kwamba siku ya tukio Meneja alikuwa ofisini ili hali washtakiwa wengine walidai kuwa hawakuwepo eneo la tukio.
Hata hivyo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite alimaliza kusoma hukumu hiyo kwa kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka kukata rufaa kwa mujibu wa sheria kutokana na kuwa wazi kama hawakuridhika na hukumu.
Picha na Ezekiel Kamanga 
Mbeya yetu

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako