A

A

Exclusive: Gardner Habash aelezea jinsi alivyokishuhudia chumba cha gereza alipofungwa Mandela (Audio)

Mtangazaji wa kipindi cha Maskani cha 100.5 Times Fm, Gardner G. Habash aka Captain ameelezea jinsi anavyomkumbuka rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Captain G. Habash ameiambia tovuti ya Times Fm kuwa aliwahi kulitembelea gereza alilofungwa Mandela , Robben Island huko Afrika Kusini, na kushuhudia chumba alichokua akishikiliwa.
“Nimewahi kutembea South Africa na nikafika kwenye mji wa Cape Town, na kule niliwahi kutembelea sehemu moja ambayo ni gereza la Robben Island, alipowahi kufungwa na kushikiliwa Nelson Mandela kwa muda mrefu sana. Pale nilipata nafasi ya kuona kile chumba ambacho alikuwa akilala Mandela, na mazingira magumu ambayo alikuwa akiishi,” amesimulia Gardner.
“Tulipata hadithi pia ya jinsi ambavyo alikuwa akiteseka katika harakati za kufanya ukombozi wa kupigana vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.” Gadner amesema pamoja na kushuhudia sehemu ya mazingira magumu na kusimuliwa mateso aliyoyapata Mzee Mandela, alishangaa kuona baada ya kutoka alikubali kusamehe na kusahau.
“Lakini kitu kikubwa ambacho nilistaajabu ni vile ambavyo alipitia Mandela, lakini baada ya kutoka akakubali kusamehe na kusahau kila kitu na kuunda taifa moja lenye manufaa kwa wa-South Africa wote, taifa ambalo aliliita Rainbow Nation kwa maana kwamba ni taifa la watu wa rangi zote. Taifa ambalo litakuwa ni kwa ajili ya wa-South Afrika pamoja na maslahi ya wa-South Africa,” ameongeza Gardner.
Amesema matendo ya Mandela yanamtofautisha na viongozi wengine wengi duniani, na kwamba anaamini kwamba yeye ndiye kiongozi bora zaidi kwa karne hii, mwenye hekima, busara pamoja na karama ya Mwenyezi Mungu.
“Naungana na South Africa, Afrika nzima pamoja na dunia kutoa heshima zangu kwa Mzee Nelson Mandela pamoja na familia yake.”

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako