Ziara ya Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk. Willbroad Slaa, imekumbwa na vurugu wilayani
Kibondo baada ya vijana kuingilia mkutano wake wa hadhara wakiwa na
mabango.
Vurugu hizo zilisababisha vijana 12 kutiwa mbaroni na polisi.
Mabango hayo
yalikuwa yakipinga hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu (CC) ya Chadema
kumsimamisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Vijana hao wakike
na kiume waliingia na mabango katika mkutano huo uliofanyika katika
kijiji cha Mabamba jimbo la Muhambwe linaloongozwa na Felix Mkosamali wa
NCCR Mageuzi muda mfupi baada ya msafara wa Dk. Slaa kuwasili kijijini
hapo.
Vijana hao
waliokamatwa na kupandishwa katika gari la polisi PT 1832 na kupelekwa
kituo kikuu cha polisi Kibondo ni Yoli James, Fasha Alex, Mohamed Hamis,
Laila Hamis, Nuru Yusuph na Mateso Mkwashu.
Wengine ni Bahati Salum, Shakuru Mahusen, Awadhi Hassan, Muliliye na Bulikoko.
Hii ni mara ya
pili kwa vijana kujitokeza na mabango katika mkutano wa Dk. Slaa ambapo
juzi ilijitokeza wilaya ya Kakonko na vijana wanne waliingia na mabango
yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali.
Katika tukio la
jana, mabango hayo yalikuwa yameandikwa ujumbe kama "Bila Zitto Chadema
ni chama cha wachaga sio makabila mengine", "Tumekuachia chama, Acha
ukabila,” "Bila Zitto Chadema hamna jipya ni sawa na nyumba bila msingi
itashuka muda wowote kuanzia sasa.”
Mengine
yaliandikwa: "Wewe siyo mwema hutufai", "Tunamtaka mtetezi wetu Mhe.
Zitto ndiyo kiongozi bora siyo wewe", "Chadema bila Zitto haiwezekani
ila Zitto bila Chadema inawezekana, Acha udini.”
Mabango mengine
yalikuwa na ujumbe kama "Imedhihirisha kuwa Chadema ni chama cha wachaga
siyo makabila mengine na Tumegundua migogoro ya udini imeanzia kwako
wewe siyo kiongozi bora hutufai.”
Polisi waliokuwa
wakilinda mkutano huo walianza kuwaondoa eneo la mkutano lakini Dk. Slaa
aliwataka askari hao kuwaacha na kutaka wasogee mbele na mabango yao
karibu na meza kuu.
Kutokana na
vurugu hizo Dk. Slaa alilazimika kwenda mbele ya jukwaa na kuanza
kueleza kuwa mkutano huo upo kwa mujibu wa sheria, aliagiza polisi
wawakamate jambo ambalo lilitekelezwa haraka.
Dk. Slaa
alimwagiza Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kibondo, Clavery Ntidyicha,
kufungua kesi dhidi ya vijana hao kwa kufanya vurugu katika mkutano kwa
niaba ya chama na kuahidi kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.
Baadaye
akizungumza na wananchi katika mkutano huo, Dk.Slaa alisema tabia ya CCM
kupandikiza isifikiri kuwa inawajenga bali watambue kuwa inawabomoa.
Alisema ameagiza
polisi vijana hao wachukuliwe hatua kwa sababu ndiyo sheria
inavyoelekeza na kwamba kama yupo mtu aliwapa pombe ili wafanye vurugu
atahukumiwa mbele ya Mungu.
Dk. Slaa alisema
katika maeneo (majimbo) atakayotembelea mkoa wa Kigoma watakaokuja na
mabango watapaswa kueleza mabango yameandikwa wapi katika katiba ya
Chadema.
Chanzo: Gazeti la Nipashe.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako