Michael Richard Wambura
BBA(Hons),
PGD-LAW, MBA(UDSM)
P.O. Box 22557
Mobile: +255-713-326485
Dar-es-Salaam
Tanzania
Fax
+255222666990
Email: michaelwambura@yahoo.com
TAARIFA KWA VYOMBO HABARI 30/NOV/2013
YAH: UTEUZI WANGU WA KUWA MJUMBE
WA KAMATI YA UTENDAJI NA MUSTAKABALI WA
MGOGORO NA SINTOFAHAMU NDANI YA SIMBA SPORTS CLUB.
Hivi karibuni niliteuliwa na Mwenyekiti wa Klabu
ya Simba Mhe Ismail Aden Rage kuwa
mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba.Wanachama na wapenzi wengi wa Simba kutoka
sehemu mbali nje na ndani ya nchi walinipiga
simu, wengine wakinitaka nikatee uteuzi na wengine wakinitaka nikubali uteuzi,
kila mmoja akiwa na sababu zake, Wakati napokea uteuzi huu na kutafakari ilibidi
nijiridhishe katika mambo mbalimbali yakiwemo yafuatayo:
1.
Uhalali wa uteuzi huu kisheria na
hasa kwa kuzingatia hali
halisi ya sasa ya siasa za Klabu.
2.
Nini mantiki ya kuteuliwa
kwangu wakati huu wa mgogoro na nini
hasa nafasi yangu.
3.
Nini utakuwa mchango wangu katika kamati ya Utendaji katika wakati huu
na baadaye.
4.
Wajibu wangu ni nini kama mwanachama wa Simba.
5.
Nini chanzo cha mgogoro huu wa Simba na ulazima wa wanachama wa Simba
Kuingia Katika Mgogoro huu.
6.
Utayari wa pande mbili zinazopingana kurudi katika meza ya Mazungumzo
7.
Athari za muda mfupi na Mrefu kwa Klabu ya Simba kwa kurejea migogoro mbali mbali iliyo wahi kutokea katika siku za Nyuma.
8.
Kina nani hasa watakaofaidika zaidi na mgogoro huu (viongozi wa Simba, Wanachama
wa Simba, Klabu ya Simba au wapinzani na
maadui wa Simba).
9.
Nini Nafasi ya TFF katika kutatua na Kupatia ufumbuzi wa mgogoro huu.
Baada ya kujiuliza na kutafakari nilitambua na
kujiridhisha kama ifuatavyo:
1.
MAMALAKA YA MWENYEKITI KUTEUA WAJUMBE WAWILI WA
KAMATI YA UTENDAJI YA SIMBA
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba Ibara ya 28(1)(d)
mwenyekiti anaweza kuteua wajumbe wawili kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya
Simba , bila kutoa nafasi ya Wateuliwa
kuuliza wameteuliwa kutoka katika kundi lipi kati ya Wajumbe wawili. Kwa
mantiki hiyo mwenyekiti anapewa nguvu za
kikatiba kuteua wajumbe wawili ambao anaona wanaweza kumsaidia katika
shughuli mbalimbali za kuendesha klabu
na sio zawadi au shukurani kama ambavyo wengi wamekuwa wakitafsiri,nadhani
jambo muhimu la kuhoji ni wanaoteuliwa wanakwenda kufanya nini kwenye kamati ya
Utendaji kwa maana ya uwezo wao kuisaidia Simba na sio nani ateuliwe na nani
asiteuliwe kwani hilo liko katika mamalaka ya
mteuzi alimradi tu anayeteuliwa ni mwanachma wa Simba na ataongeza tija
kwa klabu.
2.
NINI MANTIKI YA KUTEULIWA KWANGU KATIKA WAKATI HUU WA MGOGORO NA NINI HASA NAFASI YANGU
Wanachama na wapenzi wengi wa Simba walitafsiri
uteuzi huu umefanyika kwa nia ya kumsaidia mwenyekiti ili aendelee kukaa
madarakani, watu wenye mawazo hayo pamaoja na wengine waliokuwa na mawazo tofauti na hayo hawakuangalia na
kuzingatia kwa upana sababu za uteuzi huu,
Ukweli ni kwamba wajumbe wote wa kamati ya Utendaji ya Simba akiwemo mwenyekiti
walikuwa ni sehemu ya mgogoro huu hivyo isingekuwa rahisi pande zinazopingana kutafuta suluhu kama itahitajika, hivyo ni
wazi ni mtu mwingine mwenye uzoefu
na uwezo wa kutatua mgogoro huu na ambaye hakuwa na upande wowote katika mgogoro
huo alihitajika , aidha ninamini kuwa Uzoefu
wangu katika uongozi wa mpira wa miguu na Elimu
yangu Ulifaa kuingia katika
Kamati ya Utendaji ya Simba ili pamoja na mambo mengine niweze kutafuta na
kurejusha amani katika Simba , ninapenda ieleweke kuwa katika mgogoro huu mimi
sikuwa na sina pande wowote katika pande mbili zinazopingana , jambo lililonifanya kujiuliza ikiwa nitakubali uteuzi huu Simba Itafaidika na nini na kama nikikataa
uteuzi Smba itapata hasara kiasi gani,
niligundua kukataa kuna athari kubwa zaidi kwa Simba aidha ingekua pia ni
udhaifu na kukosa ukomavu katika uongozi ambao kwa kiasi kikubwa uamuzi huo
ungetafsiriwa ni kuweka mbele ubinafsi badala ya maslahi ya walio wengi na
klabu, watu wengi walijiuliza inakuwaje Rage
kumteua Wambura na mimi kukubali
kufanya kazi nae hasa ukizingatia
mahusiano yao katika siku za nyuma katika utawala wa mpira wa miguu, Jibu langu
ni kuwa
SIMBA KWANZA MAHUSIANO YA MTU NA MTU
BAADAYE.
3.
NINI UTAKUWA MCHANGO WANGU WA SASA NA SIKU ZA
BAADAYE KWA SIMBA.
Baada ya kutafakari kwa kina mchango wangu kama mjumbe wa kamati ya
Utendaji ya Simba kwa siku za usoni, niligundua ya kuwa sitakuwa na msaada
wowote kwa klabu yangu kama mgogoro huu hautakwisha na viongozi kurudi katika
meza moja na kufanya kazi ambayo wanachama wa Simba walitegemea wafanye wakati
wanawachagua, hivyo niliona ni vyema
nikachukua jukumu la kuingilia kati mgogoro huu ili niweze kujua nini hasa kiini cha mgogoro huu katika
Uongozi wa Simba. Nilipata nafasi ya kuongea na Mwenyekiti wa Simba na kisha kuongea na mjumbe mmoja moja
waliochaguliwa wa Kamati ya Utendaji na
Kisha kukutana nao kwa pamoja katika siku tofauti tofauti, ili kujua kiini na
sababu za sintofahamu iliyokuwa inaendelea ndani ya Uongozi wa Simba, Kwanza
nina penda kuwashukuru wajumbe wote wa
kamati ya Utendaji ya Simba Kwa Ushirikano mkubwa na mzuri walionipa, ufahamu
wao na uelewa wao wa masuala ya Simba
umeonyesha ukomavu mkubwa na weledi katika uongozi wa Simba, tumefanya mazungumzo
marefu , makubwa na ya Kina juu ya mstakabali wa Klabu yetu, wajumbe walikuwa na masikitiko na manung’uniko
mbalimbali ya msingi ambayo kimsingi mwenyekiti atakaporejea atakutana na
kamati yake ili mamabo ya msingi yaliyozungumzwa yafanyiwe kazi na kupanga
utekelezaji wake. Mwenyekiti ameisha taarifiwa
juu ya auamuzi huu. Msingi wa mazungumzo
yetu uliegemea zaidi athari ambazo Klabu yetu ingeezipata katika kipindi hiki
kuelekea ligi Mzunguko wa pili na mchezo kati yetu na Mahasimu wetu YANGA
katikati ya mwezi wa December pamoja na
athari nyingine ambazo klabu yetu
ingepata kimapato kupitia wadhamini na
wafadhili mbali mbali walio na mikata na wasio nayo, aidha wapenzi na wanachama
wengi wasiopenda migogoro wameamu kukaa
mbali na Timu yetu viwanjani na nje ya uwanja, aidha wapenzi wengi wa Simba
wamepoteza ujasiri wa kuizungumzia na kuitetea Klabu yao mitaani popote walipo
kwa kuwa hawajui siku inayofuata kutatokea
jambo gani litakalo wakarahisha, kwa kuzingatia hayo yote ndio maana
wajumbe wakaridhia mazungumzo ya kutafuta amani na umoja katika klabu yaendelee
na sasa anasubiriwa mwenyekiti ili nae atumie busara zake kumaliza mvutano huu
ambao kwa sasa umeisha fikia tamati kati ya 85%-90%.
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba Ibara 28(1)MUUNDO WA
KAMATI YA UTENDAJI “Kamati ya Utendaji inaundwa na Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti na wajumbe waliochaguliwa na
Mkutano Mkuu pamaoja na wajumbe walioteuliwa”aidha ibara hiyo inasomeka pamoja
na ibara ya 33(1)&33(3)a,b,c,d,e,f,g,h. Kwa mantiki hiyo bila Mwenyekiti
hakuna Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti bila wajumbe hakuna Kamati ya utendaji
jambo ambalo lingepelekea Simba kusimsmisha shughuli zote kwani shughuli zote
za Simba muhimu zitafanyawa na kuidhinishwa na kamati ya Utendaji kwa mujibu wa
katiba ya Simba ibara ya 30(1)a,b,c,d,e,f,g,h,i,j,k,l,m.
Aidha katika kuendeleza nia ya kuifanya Simba Moja
nitajitahidi katika siku za hivi karibuni nikitane na wanachama wa Matawi ambayo yanaonekana au kuhisiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na uongozi wa
Simba kama (Mpira Pesa, Vuvuzela na mengine) ili kujua sababu za kutokuwa na
mahusiano Mazuri na uongozi ili kutafuta suluhisho la kudumu na hatimae
washirki katika shughuli za klabu na
kuifanya Simba Moja isiyokuwa na wanachama wenye matabaka kwa sabau
yoyote ile.
4.
NINI WAJIBU WANGU KAMA MWANACHAMA WA SIMBA
Wajibu wangu wa uwanachama kama walivyo wanachama
wengine ni wa hiari kwani kila mmoja
wetu alichagua kuipenda Simba kwa hiari yake bila Shuruti lolote na bila kujali
atapata nini kibinafsi aidha kimaslahi au kiuongozi zaidi ya furaha na
maendeleo ya Simba, hivyo kila
mwanachama anawajibu kikatiba na kikanuni kuilinda , kuitumikia na kuiteteta
klabu ili ifikie malengo bila kuvunja taratibu na misingi tuliojiwekea,
inasikitisha kuona siku hizi kuna baadhi ya watu wako hiari kuona na
kusababisha timu ifungwe eti tu kwa kuwa hampendi kiongozi Fulani aliyeko
madarakani, hiyo haikubaliki na ninawaomba wanachama na wapenzi wa Simba ikiwa
watambaini mtu wa aina hiyo Katika klabu yetu ashughulikiwe mara moja , kwani
kuna watanzania wengi na wapenzi mbali
mbali wa Simba nje na ndani ya
Dar-es-salaam(MARA , MTWARA,MANYARA, SONGEA nk) ambao hawajui nini kinachoendelea
hapa ila wanaumia sana timu inapofanya vibaya katika michezo mbalimbali.
Kuhujumu klabu sio tu kwa kufungisha timu bali hatu kununua na kuuza vifaa bandia vya michezo vinavyojitambulisha
na klabu huku ukijua wazi klabu haipati mapato yoyote wote hawa wanastahili adhabu sawa na stahiki,
kutokana na matukio mbalimbali ya kujaribu kuondoa viongozi kabla ya muda wao
wa uongozi kuisha na bila mafanikio inapashwa
kuwa somo tosha kwa wanachama kuwa makini wakati wa uchaguzi kuchagua viongozi
wanaowafahamu uwezo wao bila kurubuniwa kwa zawadi na pesa ndogo ndogo, kwani
katika mfumo wa dunia ya leo sio tu kwenye Siasa hata katika mpira kuanzi
FIFA,CAF,TFF mapinduzi yamefutwa na hayakubaliki tena kwa sababu yoyote ambayo
iko nje ya utaratibu wa kikatiba.
Mwanachama
unamchagua kiongozi awe madarakani kwa miaka 4 ambayo ni sawa na siku 1460,
ukifanikiwa kuuza kura yako kwa Shs 50,000 wakati wa uchaguzi ni sawa na kuuza na kulipwa shilling 34.24 kwa siku ambayo haikutoshi hata nauli ya kuja mjini
huko ni kuhujumu klabu kama wengine,
nawaomba wanachama wenzangu tuamke tutoke kwenye usingizi huo usioleta tija
wala maendeleo na mwisho ni migogoro isiyokwisha katika klabu.
5.
NINI CHANZO CHA MGOGORO HUU WA SIMBA NA ULAZIMA WA WANACHAMA WA SIMBA KUINGIA KATIKA MGOGORO HUU.
Baada ya kuongea
na pande zote mbili katika mgogoro huu nimebaini sababu kubwa za mgogoro ni:
(i)
Mawasiliano(communication) hafifu ndani ya kamati ya utendaji jambo
linalosababisha baadhi ya wajumbe kutokujua baadhi ya mambo
(ii)
Kukosekana kwa Dira na mwelekeo
(Vision) jambo linalofanya kamati ya utendaji wote au mmoja mmoja kukosa
mwongozo wa kujua wapi klabu inaelekea.
(iii)
Kukosekana kwa uamuzi wa pamoja na uwazi (collective Decissions and
Transparence) katika baadhi ya mambo katika uendeshaji wa klabu.
(iv)
Kukosa kuaminiana (Trust) miongoni mwa wajumbe wa kamati ya utendaji
(v)
Kukosekana kwa Kanuni (regulations) mbalimbali za uongozi na Utawala,
usimamizi wa Fedha, nk.
(vi)
Kukosekana kwa mafuzo, warsha , semina na kozi mbali mbali za utawala
kwa kamati ya utendaji ili kila mmoja ajue wajibu na mipaka ya madaraka yake katika Klabu.
Baada ya kubaini
mapungufu hayo, niliona hizi ni
kasoro ambazo zinaweza kurekebishika ndani ya kamati ya utendaji yenyewe ikiwa
pande zote zinaweza kukiri mapungufu haya na kutenga wasaa na rasilimali ili
kuondoa kasoro hizo.
Kuhusu wanachama kuingilia mgogoro huu nina amini
wanachama wana nafasi yao katika kuleta na kutatua migogoro mbalimbali, lakini
katika mgogoro huu wa sasa ulikuwa kati ya mwenyekiti na Wajumbe wake wa Kamati
ya Utendaji, hivyo ilikuwa mapema mno kwa wanachama kuingilia mgogoro huu kwa
sababu bado ulikuwa ndani ya uwezo wa kamati ya utendaji ya Utendaji ya Simba.
6.
UTAYARI WA PANDE MBILI ZINAZOPINGANA KURUDI KATIKA
MEZA YA MAZUNGUMZO
Baada yakuwasiliana na kukutana na pande zote
mbili za mgogoro huu, ninapenda kuzishukuru kwa kukubali kukutana ili kumaliza
tofauti zao, ni wazi kwenye usuluhishi ni lazima pande zote zitapata na
kupoteza kiasi cha matarajio yake sio rahisi upande mmoja ukapata ilichohitaji
yenyewe kwa 100% hivyo ni wazi pande zote
kwa kuzingatia umuhimu wa mapatano kwa mustakabali wa Simba Watakaa na
kukubaliana kuondoa tofauti zao na kisha kila pande utafuata na kuheshimu katiba na kanuni kama muongozo katika
kufanikisha malengo ya Simba, mwisho wa usuluhishi hakuna upande utakao kuwa
umeshinda au kushindwa isipokua Simba
ndio itashinda, ni imani yangu watatambua nje ya Simba hakuna
aliyemaarufu miongoni mwao, na pia nana penda kuwashauri wapambe wa pande zote
kujiepusha na kutoa maneno ya kuudhi na
kejeli kwa upande mwingine ili kujenga umoja katika Simba.
7.
ATHARI ZA MUDA MFUPI NA MREFU KWA KLABU YA
SIMBA KWA KUREJEA MIGOGORO MBALI MBALI
ILIYO WAHI KUTOKE KATIKA SIKU ZA NYUMA.
Mgogoro wowote una matokeo Chanya au Hasi (+ve or
–ve results) wakati mwingine migogoro imesaidia kuwakumbusha watawala umuhimu
wa kuwatawala watawaliwa kama walivyo
kubaliana kupitia Katiba lakini wakati mwingi migogoro inaishia kuboma kama
ilivyo kuwa kwa Yanga kuzaliwa Pan Africa na kwa Simba Kuzaliwa Red Star, hivyo
ni jukumu la wahusika kupima kabla ya kuingia katika mgogoro juu ya matokeo
yake ya mwisho, kumbukumbu zangu zinanionsha hakuna kiongozi aliyewahi kupita
Simba bila migogoro kutokea na hakuna hata mgogoro mmoja uliowahi kuleta
matokeo chanya zaidi ya kurudisha nyuma maendeleo ya simba, baadhi ya migogoro
ilipelekea hadi baadhi ya viongozi
kupoteza maisha(marehemu Mzee Juma Salum na mhasibu wa Simba) wakiwa safarini wakijaribu kumaliza mgogoro,
baadhi ya viongozi wa Simba waliokutana na migogoro ni
pamoja na Mzee Hassan Brashi,Marehemu Ngonya, Marehemu mzee Bamchawi,Mzee Hazali,Mzee Chamshama, Mzee
Dalali na wengine wengi ambapo migogoro yote hiyo haikuisaidia wala kuleta tija kwa Simba, kuna wakati Simba
ilikaa karibu ya miaka mitatu bila ya
kuwa na uongozi wa kuchaguliwa Kisheria. Hivyo ni wajubu wa wana Simba tupime
na tuamue kama mgogoro huu una tija hasa ukizingatia muda wa uongozi huu
inaishia mwezi wa 5(may) 2014 na uchaguzi kufanyika, rai yangu kwa wanasimba
kufikiria, kumpima na kutafakari ni kiongozi gani tuna muhitaji kutaongoza kwa
miaka 4 ijayo kuanzia 2014 badala ya kusinzia na kuamka wakati wa uchaguzi na
kuchagua mtu asiye sahihi na baada kujaribu
kumng’oa kwa kupitia mlango wa nyuma, “mke mzuri hupewa na mwenyezi Mungu ila kiongozi mbovu humchagua wewe
mwenyewe na mungu hukubariki ukae nae kwani umemchagua mwenyewe kwa hiari
yako”.
8.
KINA NANI HASA WATAKAOFAIDIKA ZAIDI NA MGOGORO HUU
(VIONGOZI WA SIMBA, WANACHAMA WA SIMBA, KLABU YA SIMBA AU WAPINZANI WA SIMBA)
Kimsingi wanaoipenda na kuitakia mema Simba
hawawezi kwa njia moja au nyingine kufurahia migogoro ya Simba kwani inatia
maudhi na kukatisha tamaa ninaamini hata wanachama wengi binafsi hawapendi hali hii, ila kuna baadhi ya watu wachache
hawasemi ila wanafaidika binafsi
kimapato na hali ilivyo sasa na wakati mwingine wa migogoro, viongozi wa
Simba hawana faida na migogoro hii kwani inawafanya washindwe kufanya kazi
waliyowaahidi wapiga kura wao wakti wa uchaguzi.
Wanaofaidika kwa kiwango kikubwa na mgogogro wetu
ni mahasimu na wapinzani wetu kwani wana
hakika bila umoja, mshikamano na upendo hatuwezi kuwa na timu ya Ushindani,
hivi sasa timu yetu iko nafasi ya 4 mgogoro huu ukiendelea unaweza kutupeleka
pabaya zaidi hata kufika kushuka daraja, wanaokumbuka historia ya Simba wakati wa Marehemu J.D.Ngonya, tuliwahi
kuponea kushuka daraja mechi ya mwisho ya ligi sababu ya migogoro, na wakati
ule upinzani haukuwa mkali kiuchumi na kimiundombinu ya mpira kama wakati huu, hivyo wana Simba tusitumiwe na kutumia mikono
yetu wenyewe kuivunja klabu yetu, tupambane na adui wa nje halafu ndio
tuulizane wenyewe tukiwa ndani hakuna haja ya kuchochewa na maadui zetu na
kisha
kuyatangaza
matatizo yetu hadharini halafu tunaona ujiko, sifa na ufahari, hii ni hatari
kwa Klabu hasa katika biashara kwa maana ya uwekezaji na udhamini kwani hakuna mfanyabiashara anayependa kuwekeza
mahali kwenye fujo na kusiko na utulivu.
9.
NAFASI YA TFF KATIKA KUTATUA NA KUPATIA UFUMBUZI
WA MGOGORO HUU.
Simba ni mwanachama wa TFF ambapo TFF ni mwanachama wa FIFA,
kimsingi chombo kikuu kinachosimamia
Mpira wa Miguu hapa nchini ni TFF hivyo katika mfumo wa uongozi na uendeshaji
wa mpira duniani kila nchi ina chombo kinacho tambuliwa na FIFA katika
kusimamia mpira wa miguu katika nchi mwanachama hivyo kwa Tanzania ni TFF , kwa mantiki hiyo kupingana na TFF
kunaweza kuleta hatari na madhara makubwa zaidi kwa Simba, kwani TFF haiwezi
kuifutia Simba usajili wake ila inaweza kuisimamisha au kuifukuza
uanachama pale inapoona inapingana na
maamuzi yake, mfano ulitokea kwa
Tanzania kufungiwa na FIFA 2000 baada ya kukataa maagizo ya FIFA japo wakati
huo FAT ilikuwa na katiba yake, mwaka 2004 Fifa ilifupisha kipindi cha uongozi
wa FAT kutoka miaka 4 hadi 3 kwani uchaguzi ulikuwa ufanyike 2005 kama katiba
ya FAT/TFF ilivyo kuwa inaelekeza, hivyo sio busara kwa Simba ambaye ni
mwanachama wa TFF kupingana nayo,Katiba ya Simba Ibara ya 11(1)f inazungumzia Wajibu wa Mwanachama “Asiwe na
uhusiano wowote wa kimichezo na wanachama waliosimamishwa au kufukuzwa” na hata
katiba ya TFF inacho kifungu hicho hivyo Simba inaweza
kujikuta katika kisiwa ikiwa itatengwa na TFF. Kwa
kuwa suluhisho linaelekea kupatika ni matarajio yangu kuishirikisha TFF katika
kufikia makubaliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya suluhu . Ni matumaini yangu wahusika watanielewa kwani
huu ni mtazamo wangu binafsi bila kushauriwa na upande wowote na ambao hauna lengo la kuusaidia upande wowote
wa mgogogoro huu zaidi ya kuzingatia maslahi na mustakabali wa Simba Sports
Club kwa Sasa na kwa siku zijazo, ni matumaini yangu Viongozi na Wanachama wa
Simba watachukulia maoni haya kama changamoto na sio vinginevyo, na kwa wale
ambao wengependa kuhukumu basi vyema kwanza kuzingatia yafuatayo i):
Laws(sheria zilizopo),ii) Evidence(Ushahidi uliopo) na Iii) Facts of the matter(Uhalisia wa jambo)
MUNGU IBARIKI SIMBA,
MUNGU IBARIKI TANZANIA.
AHSANTENI
Michael
Richard Wambura.
Nakala:
:Mwenyekiti Simba Sport club
:Rais-TFF
Wajumbe
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako