A

A

Askari wa KMKM Zanzibar anaswa na kete 270 za Madawa ya kulevya...!!

JESHI la Polisi Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya limemtia mbaroni askari wa Kikosi cha KMKM, Hussein Soud Hussein (30) baada ya kukamatwa na dawa za kulevya jumla ya kete 270 katika eneo la Darajabovu mjini Zanzibar.
Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Upelelezi na Makosa ya Jinai Yussuf Ilembo alithibitisha kukamatwa kwa askari huyo na kusema inasikitisha sana kuona askari ambaye ndio tegemeo la kupambana na vita dhidi ya dawa za kulevya anajishughulisha na biashara hiyo haramu.

Ni kweli tumemkamata kijana mmoja Hussein Soud Hussein ambaye baada ya kumfanyia usaili alikiri na kuthibitisha kwamba yeye ni askari wa Kikosi cha KMKM na tuliona kitambulisho chake,” alisema Ilembo. 

Ilembo alisema askari huyo alikamatwa ikiwa sehemu ya msako unaoendelea wa Jeshi la Polisi pamoja na Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya kuwatafuta wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo. 

Kukamatwa kwa askari huyo kunatokana na taarifa kutoka kwa raia wema ambao walichukizwa na tabia yake ya kufanya biashara ya dawa za kulevya wakati akiwa askari wa ulinzi.

Alisema kwa sasa Polisi wapo katika doria endelevu ya kuwatafuta vijana wanaofanya biashara ya dawa za kulevya katika maeneo ya mjini na vijijini.
Taarifa zaidi ziliopo sasa kwa mujibu wa Jeshi la Polisi ni kwamba biashara ya dawa za kulevya hufanywa zaidi vijijini kutokana na msako wa Polisi Jamii ulioshamiri mjini ambao hautoi nafasi kwa wafanyabiashara hao kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa. 
Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako