MWANAMKE mmoja mkazi wa kijiji cha Mahango kata ya Madibila wilayani
Mbarali mkoani Mbeya aliyefahamika kwa jina la Jitihada Mamga(20)
ameuawa kwa…
MWANAMKE mmoja mkazi wa kijiji cha Mahango kata ya Madibila wilayani
Mbarali mkoani Mbeya aliyefahamika kwa jina la Jitihada Mamga(20)
ameuawa kwa kuchomwa kisu na mumewe aliyefahamika kwa jina Gervas Kadaga
(25) ambaye pia ni mkazi wa kijijini hapo.
Tukio hilo limetokea Novemba 21 majira ya saa 1:00 jioni baada ya
kutokea ugomvi baina ya wapenzi hao ambapo marehemu alikutwa na majeraha
tisa ya kisu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Diwani Athumani alisema kuwa
marehemu alifia nyumbani kwake ambapo mtuhumiwa ambaye amelazwa katika
hospitali ya Rufaa Mbeya naye amejeruhiwa kwa kuchomwa na kisu tumboni.
Hata hivyo Kamanda Athumani alisema kuwa hadi sasa hakijafahamika
chanzo halisi cha ugomvi huo ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kufanya
uchunguzi wa tukio hilo huku mtuhumiwa akiwa amewekwa chini ya ulinzi wa
polisi katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya alikolazwa.
Akizungumza katika hospitali ya rufaa alikolazwa, mama mkubwa wa
Gervas aliyejitambulisha kwa jina la Martha Lugenge alisema kuwa vijana
hawa walikutana Madibila kila mmoja akiwa katika shughuli zake ndipo
walipoamua kuishi pamoja.
Alisema yeye alipewa taarifa za tukio hilo siku iliyofuata na kwamba
alipofika alikuta ndugu wa marehemu wameuchukua mwili wa mtoto wao kwa
ajili ya taratibu za mazishi na kwamba hajui chanzo cha ugomvi
uliosababisha wapigane visu.
Mama huyo alisema kuwa vijana hao hawajawahi kupata mtoto na kwamba
hawajaanza kuishi pamoja muda mrefu; ''Wote ni watoto, kwani wameanza
kuishi muda mrefu? wamekutana kila mmoja akiwa katika kazi zake, ndipo
walipoanza kuishi kama mke na mume,'' alisema
(HABARI / PICHA: Mbeya Yetu Blog)
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako