A

A

UNDANI WA MTANZANIA ALIYEKAMATWA SAKATA LA UGAIDI KENYA

Mtuhumiwa ugaidi Kenya alitoweka shuleni Dodoma

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bihawana mkoani Dodoma, Joseph Mbilinyi akizungumza na mwandishi wa Mwananchi kuhusu mwanafunzi wa kidato cha tano shuleni hapo, Rashid Mberesoro (kulia) ambaye anahusishwa na tuhuma za ugaidi nchini Kenya. Picha na Sharon Sauwa      
Kwa ufupi
Habari zilizothibitishwa na wazazi wake ni kuwa mwanafunzi huyo anasoma katika Shule ya Sekondari ya Bihawana, Dodoma, baada ya kufaulu katika Shule ya Sekondari Gonja mkoani Kilimanjaro.
Moshi/Dodoma. Mtanzania aliyekamatwa
Kenya akidaiwa kufanya ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa uliosababisha vifo vya watu 148, Rashid Charles Mberesero (20) ni mwanafunzi wa kidato cha tano, lakini uongozi wa shule anayosoma umesema alitoweka shuleni hapo Desemba mwaka jana.
Habari zilizothibitishwa na wazazi wake ni kuwa mwanafunzi huyo anasoma katika Shule ya Sekondari ya Bihawana, Dodoma, baada ya kufaulu katika Shule ya Sekondari Gonja mkoani Kilimanjaro.
Mama mzazi wa kijana huyo, Fatuma Ali alisema jana kuwa: “Baada ya kufaulu alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya Bihawana na likizo alirudi nyumbani na baada ya likizo kuisha aliniaga anarudi shuleni.”
Taarifa hizo zimekuja wakati Mberesero maarufu kwa jina la Rehani Dida, akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo jijini Nairobi baada ya watuhumiwa wengine kufikishwa mahakamani juzi.
Mwendesha mashtaka, Daniel Karuri alisema, “Rehani Dida” hakufikishwa kortini kwani alikuwa na wapelelezi mjini Garissa kukusanya ushahidi zaidi, baada ya kukiri kuwa ni mfuasi wa kundi la Al-Shabaab.
Mtanzania huyo anadaiwa kukamatwa baada ya kujificha kwa saa nane akiwa amejichanganya na maiti, lakini baadaye alipanda na kujificha darini akiwa na mabomu.
Kauli ya wazazi
Jana, mama huyo, aliliambia gazeti hili kuwa haelewi ni nani aliyemshawishi mwanaye kujiunga na kundi hilo na kwamba jambo hilo limemshtua.
“Hizi taarifa tumezisikia na kuona kwenye TV na kwa kweli zimetushtua sana, mimi nahisi huko shule ndiko alikokutana na watu wabaya,” alisema Fatuma ambaye ni mkazi wa Gonja wilayani Same.
Baba mzazi wa mtuhumiwa huyo, Charles Mberesero Temba, alikiri kuwa Rashid ni mtoto wake ambaye alizaa na Fatuma mwaka 1994 na miaka yote alikuwa akiishi na mama yake.
“Huyo mtoto sijawahi kuishi naye, muda wote tangu 1994 alikuwa akilelewa na mama yake,” alisema Temba na kuongeza kuwa hakuwahi kuishi na mzazi mwenzake huyo.
“Mwaka jana mama yake ndipo alinikutanisha na mtoto na akanitambulisha na mimi nikamshauri abadili dini kwa sababu mimi ni Mkristo Mkatoliki,” alisema.
Alisema aliendelea kuwasiliana naye na aliwahi kumpeleka kanisani mara tatu akimshauri abadili dini ili arudi kwenye dini ya baba, lakini alikataa.
Alisema inavyoonekana ushauri wake huo haukupokewa vizuri na mwanaye na huyo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mawasiliano baina yao kukatika.
Kutoka Bihawana
Habari zilizopatikana jana kutoka shuleni Bihawana zilisema kuwa Mberesero alitoroka shuleni Desemba mwaka jana, baada ya kukaidi kuvua kofia katika eneo la shule.
Mkuu wa Shule hiyo, Joseph Mbilinyi alisema alimpokea mwanafunzi huyo Agosti 15, mwaka jana akitokea katika Shule ya Sekondari ya Kigwe wilayani Bahi.
Alisema mwanafunzi huyo alipata uhamisho baada ya kubadilisha masomo kutoka masomo ya sanaa mchepuo wa Historia, Jiografia na Kiswahili (HGK) na kuingia katika masomo ya sayansi ya Fizikia, Kemia na Biolojia (PCB).
Mbilinyi alisema katika shule hiyo wanafunzi walikuwa na mazoea ya kuvaa rozali na kofia, jambo ambalo alilipiga marufuku lakini Novemba 24, mwaka jana alikutana na kijana huyo akiwa amevaa kofia.
“Nilimwambia aivue aichanechane mbele yangu, lakini alikataa na kunijibu kuwa amezoea kuivaa na hawezi kuichana. Kwa sababu ilikuwa ni usiku niliondoka na kofia hiyo na kumwambia kesho yake asubuhi aje ofisi kwangu ili tumalize suala hilo, alikuwa ni mtu wa kwanza kufika ofisi kwangu. Nilimwambia anieleze kwa nini hataki kuichana, ningeweza kumsaidia kumtafutia shule ambazo zinaruhusu mavazi hayo.”
Alisema hata baada ya mazungumzo hayo, Rashid hakueleza kwa nini alikataa kuichana ndipo alipoambiwa kuwa angerejeshwa nyumbani ili aje na mzazi wake na aichane mbele yake.
“Kwa kawaida wanafunzi wengine ukiwaeleza hivyo, huwa wanaomba msamaha yanaisha lakini kwa Rashid ilikuwa ni tofauti, aliniambia yuko tayari kurudishwa nyumbani lakini siyo kuchana kofia hiyo,” alisema.
Mwalimu huyo aliongeza: “Niliona njia ya kumsaidia ni kuwashirikisha walimu ambao wanasimamia msikiti wetu huu. Walimu walimuita na akakubali kupewa adhabu ili jambo hilo liishe bila kufikishwa kwa wazazi wake.”
Hata hivyo, alisema baada ya mazungumzo hayo, Rashid alichukua begi lake na kuondoka kwenda mjini na kuwaacha wenzake wakimalizia mtihani wa Biolojia.
“Nilipata shida sana sikupenda mwanafunzi huyu aondoke shuleni, nilitaka hili jambo lipate suluhu. Nilipigia simu alizoandikisha shule ikiwamo ya baba yake bila mafanikio kwa sababu hazikupokewa, isipokuwa moja ambayo ilipokelewa na mwanamke ambaye alikana kumfahamu.
“Hadi leo bado ni mwanafunzi wetu kwa sababu kanuni zinasema baada ya siku 90 kama mwanafunzi hajaonekana shuleni, tunapeleka jina kwenye Bodi ya Shule ambayo itatoa uamuzi,” alisema.
Katibu mstaafu wa Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu katika shule hiyo, Mungi Ramadhan Mungi alisema Rashid alikuwa ni mtu wa msimamo, akitaka jambo lake hata kama halina usahihi analisimamia.
“Aliwahi kutaka kupigana msikitini mara mbili, mara ya kwanza tulikuwa tukiuliza maswali kuhusu masomo ya darasani yeye akasema hairuhusiwi kufanya hivyo msikitini,” alisema.
Alisema hatua hiyo ilizua mabishano na alifikia uamuzi wa kutaka kuwachapa walioongelea mambo ya masomo ndani ya msikitini.
“Alikuwa ni mtu wa msikitini na bwenini mara nyingi hakupenda kuchanganyika na wenzake, jambo hilo lilimfanya hata kukosa marafiki,” alisema.
Alisema aliwahi kuwahadithia kuwa alibadili dini akiwa anasoma sekondari huko Moshi.
Mwalimu anayewasimamia wanafunzi wa Kiislamu, Mohamed Mwijuma alisema baada ya Rashid kutoroka shuleni hapo waligundua alikuwa ni mwanafunzi aliyekuwa na matumizi yasiyo ya kawaida.
“Pia tuligundua kila mwisho wa wiki alikuwa akitoroka kwenda mjini,” alisema Mwijuma ambaye alishiriki kulipatia ufumbuzi tatizo hilo la kukutwa na kofia shuleni.
Hata hivyo, alisema Februari mwaka huu, Rashid alirejea mwisho wa wiki na kuondoka moja kwa moja na mizigo yake yote.
Habari zilizopatikana shuleni hapo zilisema baada ya Rashid kutajwa kuhusika na tukio hilo, mama yake mzazi alifika shuleni hapo kumtafuta mwanaye.
Chanzo;Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako