A

A

Shyrose Bhanji ‘alivuruga’ Bunge Eala Mashariki


Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji. Picha na Maktaba 
Kwa ufupi
Bunge hilo lilianza vikao vyake Oktoba 20, mwaka huu likitarajiwa kujadili na kupitisha miswada kadhaa ya sheria pamoja na taarifa za kamati, lakini hadi jana hakuna kazi hata moja kati ya hizo iliyokuwa imefanyika kwa ukamilifu, kutokana na mgomo unaoendelea huku likitarajiwa kuhitimisha kazi zake leo.

Kigali. Kwa siku zaidi ya 10 sasa,
Bunge la Afrika Mashariki (Eala) limeshindwa kuendelea na vikao vyake mjini hapa kutokana na wabunge wake kugomea vikao hivyo vya mkutano wa pili, wakishinikiza kuchukukuliwa hatua kwanza kwa mmoja wa wabunge wake, Shy-Rose Bhanji wa Tanzania.
Bunge hilo lilianza vikao vyake Oktoba 20, mwaka huu likitarajiwa kujadili na kupitisha miswada kadhaa ya sheria pamoja na taarifa za kamati, lakini hadi jana hakuna kazi hata moja kati ya hizo iliyokuwa imefanyika kwa ukamilifu, kutokana na mgomo unaoendelea huku likitarajiwa kuhitimisha kazi zake leo.
Miongoni mwa kazi zilizokuwa zimepangwa kufanyika ni pamoja na kujadili na kupitisha muswada wa Sheria ya Ushirika wa Afrika Mashariki na kupokea taarifa za Kamati ya Masuala ya Jumuiya na Utatuzi wa Migogoro, Kamati ya Sheria, Kanuni na Haki, Ripoti ya Kamati ya Hesabu zilizokaguliwa za EAC kwa mwaka wa 2012/13 pamoja na taarifa iliyoitwa nyeti ya Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji (CTI).
Vikao vyote ambavyo vimefanyika kwa ajili ya kuliwezesha Bunge hilo kutekeleza kazi hizo, vimekuwa vikiahirishwa baada ya dakika kati ya 20 na 30 kutokana na baadhi ya wabunge kutumia kanuni ya 31 kutoa hoja ya kutaka mjadala kuhusu Bhanji ufanyike kwanza kabla ya kuendelea na shughuli nyingine.
Mjumbe wa Tanzania ambaye ni mwenyekiti wa CTI, Angela Kizigha alisema taarifa ya kamati yake haikujadiliwa baada ya wabunge kutaka kwanza suala la nidhamu lipewe nafasi. “Hiyo ndiyo hali halisi, walikataa na mimi sikuwa na jinsi ya kulazimisha,” alisema.
Gazeti hili limebaini kuwa baadhi ya wabunge wanaoshinikiza kujadiliwa kwa suala la Bhanji, wanataka kwanza aondolewe katika ujumbe wa Kamishna wa Bunge hilo na baadaye asimamishwe kushiriki katika vikao vya Eala kwa kadiri muda utakavyoamuliwa.
Juzi alasiri, Spika wa Bunge hilo, Dk Margaret Zziwa alitoa taarifa kwamba Oktoba 21 na 22, 2014 Tume ya Eala ilikutana na kujadili suala la utovu wa nidhamu wa baadhi ya wabunge wake, lakini ilishindwa kulihitimisha kutokana na ukubwa wa tuhuma husika huku akiahidi kuwa suala hilo lingejadiliwa tena jana.
“Kwa kuwa mambo yaliyohusishwa ni mazito, hayakuweza kupata hitimisho, suala hili litajadiliwa tena kesho (jana), Jumatano Oktoba 29, 2014 wakati wa kikao cha tume na hatua zitakazochukuliwa mtajulishwa,” alisema Dk Zziwa.
Tuhuma zake
Bhanji anatuhumiwa kwamba aliliaibisha Bunge hilo wakati wa ziara ya nchini Ubelgiji iliyowashirikisha wajumbe wa tume na wenyeviti wa Kamati za Bunge hilo na kwamba alifanya fujo ndani ya ndege kwa kutoa lugha chafu kwa wabunge wenzake pamoja na kutoa matamshi yasiyo ya staha katika hafla iliyoandaliwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Dk Diodorus Kamala.
Juzi baada ya kikao cha Eala kuahirishwa dakika 30 tangu kilipoanza, wabunge wa Tanzania walikutana kwa zaidi ya saa mbili katika moja ya kumbi za Bunge la Rwanda, kujadili hatima ya mwenzao, kikao ambacho hata hivyo hakikuwa na mwafaka wa pamoja.
Mmoja wa wabunge hao, Makongoro Nyerere alisema wameshindwa kuwa na mjadala wa kina na baadaye kutoa msimamo kuhusu suala hilo kwa sababu Bhanji hakuwa amepewa tuhuma rasmi zinazomkabili, badala yake kumekuwa na malalamiko ya mdomo tu.
“Tunashindwa kutoa uamuzi wa pamoja kuhusu suala hili kwa sababu mpaka sasa Shyrose hajapewa tuhuma rasmi kimaandishi kuhusu makosa aliyofanya, badala yake watu wananung’unika tu. Sasa kwa kuwa kesho Tume ya Bunge inakutana, basi tunaweza kufahamu ukweli kuhusu tuhuma hizo,” alisema Nyerere.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Bhanji alisema: “Mimi nasikia tu na kusoma kwenye social media (mitandao ya kijamii), lakini sijapewa kimaandishi kwamba ninatuhumiwa kwa kosa hili, hili na hili. Kwa kuwa kesho (jana) kuna kikao cha tume, basi tusubiri pengine nitapewa mashtaka yangu.”
Alipoulizwa ni kitu gani kilichojiri wakati wa safari ya Ubelgiji, Bhanji alisema tuhuma dhidi yake ni za kutunga na zimejaa chuki za kisiasa ndani yake na kuthibitisha kuwa tayari alishajibu tuhuma hizo kupitia mitandao ya kijami na sasa anasubiri tuhuma rasmi katika tume ya Eala.
Kupitia mitandao ya kijamii Bhanji alikanusha tuhuma hizo akisema: “Shutuma hizi hazina ukweli wowote na zinalenga, si kuniharibia, bali kuchafua sifa yangu na utendaji kazi wangu katika Bunge la Afrika Mashariki.
Lengo kuu la shutuma hizo ni kunivunja nguvu na ari ya kutetea masilahi ya nchi yangu na Watanzania wenzangu kwani daima nimekuwa kikwazo na mwiba kwenye ajenda zinazokiuka masilahi ya Tanzania.”
Alitaja baadhi ya mambo ambayo anadai ni sababu ya tuhuma kwake kuwa ni msimamo kuhusu sera ya ardhi, kupinga mpango wa kumwondoa madarakani Spika wa EALA, Dk Margaret Zziwa ambao anasema alisimama kidete kuupinga kwa sababu haukuwa na masilahi kwa Tanzania.
Jana jioni Bunge hilo lilikuwa likimjadili Bhanji baada ya Mbunge wa Uganda, Dorah Byamukama kutoa hoja ya kujadiliwa kwake kwa kuliaibisha bunge hilo kwa utovu wa nidhamu aliouonyesha Ubelgiji.
Imeelezwa hiyo ni hatua ya kwanza baada ya hapo watachukua hatua nyingine ya kinidhamu ya kumsimamisha kwa muda wa kati ya miezi mitatu mpaka sita na pia kuvuliwa ukamishna ambao ulikuwa ukimpa nafasi ya kuingia kwenye tume ya bunge ambayo kila nchi inawakilishwa na wabunge wawili.
“Na sasa wameamua kunitukana na kuzusha tuhuma kadhaa kupitia mitandao ya kijamii ambako yote ni utunzi wa kisanii usiokuwa na chembe ya ukweli, uhalali wala ushahidi,”alisema Bhanji na kuongeza:
“ ….walete ushahidi wa tuhuma zote dhidi yangu…kwa mfano, shutuma kwamba nililewa pombe ndani ya ndege, kuvunja chupa, kufanya fujo na kufungwa pingu wakati wa safari ya Ubelgiji si kweli hata kidogo”.

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako